Waislamu kote Afrika na Duniani wanasherehekea Eid al-Fitr, inayoashiria mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Sikukuu hii inasherehekewa kwa mikusanyiko ya familia, mavazi mapya na vitafunio vitamu.
Waumini walijiunga kwa sala za jamaa bega kwa bega katika viwanja vya wazi, mitaani na ndani ya misikiti.
Nchini Chad, wanajeshi waliteremka kutoka kwenye magari yao na kuweka chini silaha zao ili kujiunga na waumini kwa sala za asubuhi.
Huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya, kundi hili la waumini lilijazana katika uwanja wa wazi eneo la Ngara kwa sala za jamaa.
Katika kijiji cha Abu Sir huko Giza, Misri, watu waliweka maputo yenye rangi za bendera ya Palestina na kukusanyika chini ya kivuli chake kufanya sala na kuwatakia Wapalestina amani, walisema.
“Eid njema, natumai siku zijazo ni nzuri. Mungu awaunge mkono ndugu zetu wa Palestina na kuwalinda. Na, Mungu akipenda, awajalie sikukuu ya Eid itakayowaletea furaha, amani na baraka.” mkazi Abdullah Mohamed alisema.