Ngais Karero ameazimia kutimiza ndoto yake ya kuwa mwanamke wa kwanza kurusha puto nchini Tanzania./Picha:Ngais Karero

Na Edward Qorro

Katika lugha ya Kiswahili, kuna msemo usemao ‘Safari moja huanzisha nyingine’.

Na ndivyo ilivyokuwa kwa Ngais Karero, binti wa Kimaasai kutoka kijiji cha Terat, wilayani Simanjiro mkoani Manyara nchini Tanzania.

Miaka 10 iliyopita, akiwa futi kadhaa angani, Karero alivutiwa na umahiri wa rubani wa puto alilokuwa amepanda wakati akiwa ndani ya hifadhi ya taifa ya Serengeti nchini Tanzania.

Karero anasema aliona kitu kingine cha kufanya maishani na utalii wa puto, ulimfungulia dunia mpya./Picha: Ngais Karero

“Nilipata fursa kumshuhudia rubani Mohammed Masudi, ambaye ni Mtanzania kurusha puto angani. Hakika nilishangazwa sana na umahiri wa rubani yule wakati akituendesha ndani ya lile puto kubwa, mara moja nilihisi kuwa hicho ndicho nachopaswa kufanya,” anasema Karero, katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Kutoka studio hadi angani

Kabla ya safari ya kujifunza urushaji wa puto, Karero alikuwa anafanya kazi kama mtangazaji katika kituo cha redio cha Orkonerei, maarufu kama ORS, kinachopatikana mkoani Manyara nchini Tanzania.

Karero anasema aliona kitu kingine cha kufanya maishani na utalii wa puto, ulimfungulia dunia mpya.

Kabla ya safari ya kujifunza urushaji wa puto, Karero alikuwa anafanya kazi kama mtangazaji katika kituo cha redio cha Orkonerei, maarufu kama ORS, kinachopatikana mkoani Manyara nchini Tanzania./Picha: Ngais Karero

“Nadhani ilikuwa ni wakati muafaka kwangu kufanya kitu kingine maishani,” anaeleza.

Kulingana na Karero, urushaji wa puto unahitaji mafunzo ya kutosha, ikiwemo mafunzo ya usalama, hali ya hewa, ufundi, sheria za anga na kadhalika.

Kazi hiyo pia inahitaji utimamu wa kimwili, kiakili na kuweza kufanya kazi chini ya shinikizo.

Ngais Karero akiwa mafunzoni nchini Uturuki./Picha: Ngais Karero

Kama mwenyewe anavyosema, urubani wa puto ni taaluma yenye kulipa vizuri tu.

“Ni taaluma nzuri, hasa kwenye masuala ya kujuiingizia kipato kwani inafanyika katika sekta ya utalii, na kila mtu anafahamu umuhimu wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi yoyote ile,” anasema.

Kwa sasa, Karero ana cheo cha rubani binafsi, akiwa amejiwekea nia ya kufikisha saa 300 hewani ili apande cheo na kuwa rubani mkufunzi.

Mafunzo nchini Uturuki

Kulingana na Karero, safari ya kuwa rubani wa puto si ya lelemama.

Ngais Karero akiwa ndani ya hifadhi ya taifa ya Serengeti nchini Tanzania./Picha: Ngais Karero

Haikuwa rahisi kwake kufikia hatua hiyo, kwani ilibidi apangiwe kazi katika idara ya rasilimali watu katika kampuni ya Nyssa Balloon Safaris ya nchini Tanzania.

“Nilikuwa nasimamia rasilimali watu kabla ya waajiri wangu kuniunga mkono ili nitimize ndoto yangu ya kuwa rubani,” anaiambia TRT Afrika.

Kulingana na Karero, kampuni yake ilimpelekea nchini Uturuki kw ajili ya mafunzo zaidi ili aweze kutimiza ndoto zake za kuwa rubani kamili.

Kwa sasa, yuko katika jimbo la Cappadocia nchini Uturuki, akipata mafunzo ya kina ya kuwa rubani mbobezi.

Anategemewa kumaliza mafunzo yake mapema mwaka 2025, wakati atakapokywa rubani kamili.

“Naishukuru serikali ya Uturuki kwa kunipa fursa hii adhimu, ambayo pia ni maono ya Rais Recep Tayyip Erdogan ambaye anatilia mkazo jambo la ushirikiano katika nyanja mbalimbali,” anasema.

Karero anaamini kuwa amefika hapo alipo kutokana na imani yake thabiti kwa Mungu na kufanya kazi kwa bidii.

Kwa sasa, ameelekeza mawazo yake yote katika kumaliza mafunzo yake ili awe rubani wa kwanza mwanamke wa puto nchini Tanzania.

TRT Afrika