Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Wakati mwaka 2024 ukielekea ukingoni, yako baadhi ya matukio ambayo yaligonga vichwa cha habari nchini Tanzania. TRT Afrika imekuandalia japo kwa ufupi orodha ya matukio hayo.
Kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, Februari 10
Siku ya Februari 10, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliagiza bendera ya taifa kupepea nusu mlingoti kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa.
Lowassa alifariki katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKIC) alipokuwa anapata matibabu ya mapafu na shinikizo la damu.
Katika taarifa yake kwa Taifa, aliyoitoa kupitia Televisheni ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), akiwa Arusha, Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango alisema kuwa Lowassa alikuwa JKCI tangu Januari 14, 2022 baada ya kurejea nchini kutoka Afrika ya Kusini alipokuwa anapokea matibabu ya maradhi hayo.
Kifo cha Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Februari 29
Wakati Watanzania bado wanaendeela kujifuta machozi ya kumpoteza Lowassa, msiba mwingine ukalikumbuka taifa hilo, kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi aliyefariki dunia Alhamisi ya februari 29, 2024 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Akitangaza kifo cha kiongozi huyo, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, alisema kuwa Mzee Ali Hassan Mwinyi alikuwa akipatiwa matibabu tangu Novemba mwaka 2023 huko London nchini Uingereza, kabla ya kurejea nchini Tanzania kwa matibabu zaidi.
Mzee Mwinyi alifariki dunia akiwa na miaka 98.
Kuanza kwa matukio ya utekaji watu, Juni 23
Baada ya kuwa yamesahaulika kwa kipindi cha miaka minne, tukio la kutoweka kwa Edgar Mwakabela, maarufu kama Sativa na baadaye kuokotwa akiwa na hajitambui ndani ya pori mkoani Katavi, liliamsha kumbukumbu mpya ya matukio hayo ambayo yaliwahi kutia dosari taswira ya taifa hilo.
Miezi miwili baadaye, ikawa ni zami ua Deusdedith Soka, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA), ambaye hadi sasa hajulikani alipo, kabla ya aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema Ali Kibao kushushwa ndani ya basi, wakati akielekea Tanga kabla hajakutwa ameuwawa siku chache baadaye.
Uzinduzi wa reli ya SGR, Agosti 1
Baada ya kusubiri kwa muda mrefu, hatimaye Watanzania walishuhudia uzinduzi rasmi wa safari za treni za abiria katika reli ya kiwango cha kimataifa yaani SGR, miundombinu ya reli na stesheni kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
Nchi hiyo ilikuwa imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani billioni 10 kwa lengo la kuboresha ustawi wa maendeleo ya wananchi kwa kasi na kupunguza gharama na muda wa usafirishaji wa mizigo na abiria kati ya maeneo hayo mawili.
Tanzania yafuzu michuano ya AFCON 2025, Novemba 19
Tasnia ya michezo, ilipokea taarifa za kufuzu michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa kufuraha, kufuatia ushindi wa timu ya soka ya taifa ‘Taifa Stars’ dhidi ya Guinea.
Hatua hiyo ilikuja wakati nchi hiyo ikijiandaa kuwa mwenyeji mwenza wa michuano ya CHAN 2024 na AFCON 2027, kwa kushirikiana na majirani zake wa Kenya na Uganda.
Hii itakuwa ni mara ya nne kwa Tanzania kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika, ikiwa imeshafanya hivyo mwaka 1980, 2019 na 2023.
Kifo cha Faustine Ndugulile, uchaguzi wa serikali za mitaa, Novemba 27
Wakati Watanzania wakijiandaa kwenda kushiriki mchakato wa kuwachagua viongozi wao katika ngazi ya serikali za mitaa, iliibuka taarifa ya kusikitisha, kuhusiana na kifo cha aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya na pia Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Kanda ya Afrika, Dkt Faustine Ndugulile.
Ndugulile, ambaye alikuwa akipatiwa matibabu nchini India, alifariki miezi michache kabla ya kushika hatamu ndani ya WHO baada ya kuchaguliwa mwezi Agosti.