Wanasarakasi Ramadhani Brothers kutoka Tanzania wasubiri ushindi katika shindano la America's Got Talent

Wanasarakasi Ramadhani Brothers kutoka Tanzania wasubiri ushindi katika shindano la America's Got Talent

Kura zitafungwa leo asubuhi nchini Marekani wakati wapiga kura kutoka Tanzania wakichagua kutumia njia kama VPN ili waweze kupiga kura kwa niaba yao.
Ramadhani Brothers Americas Got Talent | Picha: Ramadhani Borthers

Hii leo shindano la America Got Talent linatarajiwa kufikia kilele na hivyo washiriki katika fani mbalimbali kutangazwa mbele ya mamilioni ya mashabiki ambao wanafuatilia kwa karibu tamasha hilo.

Mashabiki kutoka Afrika Mashariki hasa Tanzania wanalifuatilia kwa karibu huku wakitarajia ndugu wawili wanasarakasi maarufu Ramadhan Brothers ambao ni washiriki kutoka nchi hiyo wanaweza kuibuka kidedea. .

Ramadhani Brothers, kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii, wamewahimiza mashabiki walioko nchini Marekani na kote duniani kuwapigia kura kadri wawezavyo ili wapate ushindi.

Wakati huo huo, wapiga kura kutoka Tanzania wamechagua kutumia njia kama VPN ili waweze kupiga kura kwa ajili yao kwani sheria zinasema kuwa ni watu kutoka nchini Marekani pekee ndio wanaweza kupiga kura kwa ajili ya washiriki wa AGT.

Watanzania wameamua kutumia huduma ya VPN kuwapigia kura

Jaji mmoja wa kipindi hicho cha talanta, ambae ni mwanamitindo wa zamani, Heidi Klum, jana usiku alisema kuwa Ramadhani Bros ni wa kushangaza kweli. Huku Jaji maarufu Simon Cowell aliongeza kuwa, "Nilipofikiri najua nani atashinda kipindi hiki, kila kitu kilibadilika mlivyoingia nyie."

Washiriki wengine wa fainali za AGT 2023 ni: Mzansi Youth Choir kutoka Afrika Kusini, Putri Ariani, Ahren Belisle. Murmuration. Adrian Stoica & Hurricane. Lavender Darcangelo.

Hii ni mara ya kwanza kwa nchi ya Tanzania kushiriki shindano hilo kubwa na la kimataifa ambalo hujumuisha watu kutoka mataifa mbalimbali wenye vipaji tofauti.

TRT Afrika