Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed awasili Somalia kwa mkutano na Rais wa nchi hiyo Hassan Sheikh Mohamud picha na Ikulu ya Somalia

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amewasili nchini Somalia, na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud.

" Mkutano wao unatarajiwa ''kuimarisha ushirikiano wa usalama, kuimarisha ushirikiano wa biashara, na uhusiano wa kidiplomasia," kulingana na shirika la habari la serikali ya Somalia, SONNA.

" Ziara hii inaashiria hatua muhimu ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Somalia na Ethiopia, huku viongozi hao wawili wakipangwa kushiriki katika majadiliano kuhusu masuala muhimu ya mataifa yao na kikanda yenye maslahi kwa pande zote," ikulu ya Somalia imesema.

Ziara hiyo inafuatia juhudi zinazoendelea za kuimarisha uhusiano baada ya mvutano kati ya Ethiopia na Somalia kurindima mwaka jana.

Uhusiano ulidorora baada ya Ethiopia kutia saini mkataba na Somaliland Januari 2024, ambao Somaliland ilidai ungesababisha Ethiopia kutambua uhuru wake.

Kufuatia makubaliano ya amani yaliyoratibiwa na Uturuki mwezi Disemba 2024, Ethiopia na Somalia zilitangaza kurejesha kikamilifu uhusiano wa kidiplomasia mwezi Januari.

Wakati wa mkutano wa marais na viongozi wa Afrika jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia 15 na 16 Februari 2025, viongozi hao wawili walikutana.

Wakati huo Abiy Ahmed alisema " Ushirikiano wa kuimarika unahitaji kuwa na msingi thabiti."

TRT Afrika