Tuzo hiyo ya kifahari ya Ballon D'or, bado inamkwepa nahodha huyo wa Ufaransa, ambaye alimaliza mwaka huu katika nafasi ya tatu, ambayo ni nafasi yake bora hadi sasa.
Nyota mshambuliaji wa Ufaransa Kylian Mbappe anaweza kushinda taji la kifahari la Ballon D'or akichezea "timu yoyote," Ronaldinho ameiambia AFP Jumapili, lakini Mbrazil huyo angependa ashinde na klabu yake ya sasa, Paris Saint-Germain, "timu kubwa."
Kwenye mahojiano yake na AFP nchini Thailand, wakati wa ziara yake Bangkok kama balozi wa Teqball, mchezo mpya unaochanganya mpira wa miguu na tenisi ya meza, Ronaldinho alisisitiza, "Natumaini atashinda. Yeye ni rafiki mzuri na mchezaji mzuri sana. Ninapenda mtindo wake wa kucheza."
Ronaldinho, ambaye pia ni bingwa wa Kombe la Dunia la 2002 alisema, "Mchezaji mzuri kama yeye anaweza kupata nafasi ya kushinda Ballon D'or katika timu yoyote, lakini kwa kuwa ninapenda PSG, ningependa afanikiwe hivyo na PSG."
"Kushinda mashindano makubwa kutamsaidia sana," alisema Ronaldinho, ambaye alivaa jezi namba 10 akiichezea PSG kati ya 2001 na 2003.
Mwaka ujao, 2024 unaonekana kuwa wenye shughuli nyingi na usiotabirika kwa Mbappe.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 kuna uwezekano wa kutinga fainali za Ligi ya Mabingwa, pamoja na Euro 2024 na PSG na Ufaransa.
"Kama kila mwaka, ni vigumu sana (kushinda Ligi ya Mabingwa). Lakini PSG ina kocha mzuri, wachezaji wazuri sana, na kwa hivyo, kila kitu kinawezekana," mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona na Milan alisema.
Mbappe pia anatarajiwa kujadili mkataba usio na uhakika, ambao unaweza kumuona akiondoka Paris mwezi Juni.
Real Madrid, ambayo imekuwa ikimchumbia kwa miaka kadhaa, inaonekana kuwa timu bora inayomvutia zaidi.