Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania January Makamba. Picha: January Makamba
Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa msimamo wake ni kuanza tena kwa mchakato wa amani, ukiongozwa na suluhisho ya mataifa mawili kutatua mzozo wa Israel na Palestine unaoendelea.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania January Makamba amesema hayo kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa X baada ya kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Eli Cohen.

Mapema leo nilizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Israel, Eli Cohen

"Nimesisitiza msimamo wa Tanzania kwamba kipaumbele kinapaswa kutolewa kwa kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu, hasa ulinzi wa maisha ya raia," Makamba alisema.

"Nilitilia mkazo msimamo wa Tanzania kwamba shughuli za kijeshi zisitishwe ili kuruhusu juhudi za kibinadamu zisizozuiliwa."

Makamba amesema pia alijadili suala la kuwasaka Watanzania wawili Clemence Felix Mtenga na Joshua Loitu Mollel, kati ya raia wa kigeni ambao mpaka sasa hawajulikani walipo tangu mgogoro wa Israel na Palestine ulivyoanza Oktoba, 7.

"Waziri Cohen aliahidi kujitolea kwake binafsi kwa juhudi kubwa za serikali ya Israeli kuwapata wanafunzi wawili raia wa Tanzania ambao tumepoteza mawasiliano nao tangu tarehe 7 Oktoba."

Pindi tu mzozo huo ulipozuka, mamlaka nchini Tanzania kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje, ilianzisha mpango wa kuwasajili raia wake katika ubalozi wake wa Tel Aviv ili kufanikisha taratibu ya kuwaondoa kutoka nchini humo.

TRT Afrika