''Siku ya Uhuru Tanzania tunasherehekea kwani tunaona jinsi serikali inatujali hasa wakati wa janga kama lililotukuta'' anasema mkaazi mmoja wa Hanang, aliyenusurika kutokana na maporomoko ya ardhi. / Picha : TRT Afrika 

Huku taifa la Tanzania likiadhimisha miaka 62 ya Uhuru wake, watu kutoka tabaka mbalimbali ndani na nje ya nchi wameendelea kumiminia serikali hiyo risala za pongezi ndani na nje ya nchi.

''Ni wakati wa matatizo kama yaliyotukuta juzi, ndio unajua kuwa serikali yako inakujali mno,'' amesema Gidaulanda Simbichani, mkaazi wa Hanang.

''Tunajivunia Uhuru tulionao, na serikali yetu inayotujali kwa kila jambo linalotokea wako pamoja na sisi. Ndio maana tunasema Uhuru wetu uko salama.'' Anaendelea kusema Gidaulanda.

Tangu tarehe mbili Disemba, maporomoko ya ardhi yalipotokea mkoa wa Manyara Kaskazini mwa Tanzania, viongozi mbali mbali wa serikali walikuwa wa kwanza kufika eneo hilo kuwafariji waathiriwa, huku Rais Samia SUluhu akikatiza safari yake ghafla ya kikazi mjini Dubai kutokana na uzito wa msiba huo.

Serikali ilijitolea kugharamia kila kilichohusiana na janga hilo ikiwemo mazishi kwa waliofariki na matibabu kamili kwa wote waliojeruhiwa kutokana na maporomoko hayo.

Isaya Mbise anasema yeye anaona maendeleo makubwa ya nchi hiyo ambayo ndio kikubwa zaidi analojivunia.

''Ukiangalia historia tuliopewa na wazazi wetu waliokuwepo tangu kipindi hicho tulipopata Uhuru tunaona mambo makubwa hasa miundo mbinu ya elimu, iliyowezesha wengi kupata elimu,'' ameendelea kusema Isaya.

''Kuwa huru kunakuwezesha kufanya mambo yako kwa uhuru, na bila kuvunja sheria za nchi unajiendeleza kiuchumi,'' ameongezea kusem Isaya.

Google ni miongoni mwa mashirika ya kimataifa yaliyoungana na Watanzania kusherehekea siku ya Uhuru (62) /Picha : Google

Wakati huo huo, shirika la mtandao la Google limeadhimisha siku hii ya Uhuru wa Tanzania kwa chapisho maalum la mlango wake kuingia mtandaoni.

Katika ukurasa wake, Google ilituma salamu za pongezi wa taifa nzima la Tanzania huku ikisema kuw aimeamua kuweka bendera ya nchi hiyo kwenye ukurasa wake, kuendana na halfa ya kupandishwa bendera ya Tanzania asubuhi kuashiria kupanda bendera ya Uhuru.

Rais Samia anaongoza taifa katika maadhimisho haya huku akishirikia hshughuli mbali mbali za kitaifa.

Rais Samia Suluhu amezindua mchakato wa ukusanyaji maoni kuhusu Dira ya Taifa 2050 jijini Dodoma / Picha : Ikulu Tanzania

Miongoni mwa mambo muhimu yaliyozinduliwa ni Mchakato wa ukusanyaji maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Maadhimisho hayo yamefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma 09 Desemba, 2023.

TRT Afrika