Corneille Nangaa, kiongozi wa waasi wa AFC inayojumuisha waasi wa M23 amekuwa akiongoza uasi nchini DRC. /Picha: Reuters

Hali ya mshike mshike imeshuhudiwa katika mji wa Bukavu, nchini DRC baada ya watu kadhaa kuuawa na wengine kujeruhiwa huku milio ya risasi na milipuko ikirindima katika mkutano wa hadhara uliofanywa na kiongozi wa waasi wa M23 Corneille Nangaa.

Tukio hilo limeripotiwa kutokea katika mji wa BUkavu, ulio Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo siku ya Alhamisi, kulingana na wakazi wa eneo hilo.

Picha mjongeo zilionesha watu wakikimbia barabarani huku wengine wakivuja damu, na wengine wakiokota miili.

Wakazi walisema waliona maiti, lakini hakukuwa na taarifa za haraka kuhusu idadi ya waliopoteza maisha.

Nangaa ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kuwa Rais wa DRC Felix Tshisekedi, aliamuru shambulio hilo, bila kutoa ushahidi wowote.

Hadi kufikia sasa, hakuna taarifa yoyote kutoka kwa serikali ya DRC kuhusiana na madai ya Nangaa.

Kulingana na Nangaa, yeye na wanachama wake wako salama kufuatia tukio hilo.

Kundi hilo tayari limeteka maeneo mengi mashariki mwa nchi tangu mwanzoni mwa mwaka.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, nchi jirani ya Rwanda imehusika na kuwaunga mkono waasi wa M23, madai yanayopingwa na Rwanda.

Kusonga mbele kwa waasi kumezusha hofu ya vita vya kikanda ambavyo vinaweza kushirikisha nchi jirani.

Katika hotuba yake kabla ya shambulizi hilo, Nangaa aliwaambia maelfu ya watu waliohudhuria mkutano wake wa hadhara kuwa kikundi chake kipo Bukavu kuimarisha usalama, huku likiwa limeudhibiti mji huo toka Februari 16.

"Kutakuwa na vitengo maalum na doria ambazo zitafanyika katika jumuiya zote," alisema Nangaa, ambaye alikuwa akijitokeza hadharani kwa mara ya kwanza Bukavu tangu kuchukuliwa kwa mamlaka hiyo.

Risasi zilianza kusikika mwishoni mwa mkutano, alisema mkazi mmoja. "Kulikuwa na ufyatuaji risasi kila upande. Hatujui kilichotokea. Kuna watu waliojeruhiwa, waliokufa, sijui."

M23 imekuwa ikijaribu kuonesha kwamba inaweza kurejesha utulivu katika eneo ambalo imelidhibiti kutoka jeshi la DRC, ikiwa pia imefungua bandari na shule katika eneo hilo.

Reuters