Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Haki na Ulinzi ndani ya Bunge la Afrika Kusini Jane Mananiso, amewapongeza wanajeshi wawili wa kike wa jeshi hilo ambao wamepata ujauzito licha ya kushiriki shughuli ya kulinda amani nchini DRC.
Mananiso alisisitiza kuwa hakuna aibu yoyote kushika mimba katika taaluma yoyote ile, wakiwemo wanajeshi na askari polisi wa Afrika Kusini.
“Si aibu kupata ujauzito, kimsingi ni haki ya kikatiba kwa mwanamke yeyote yule kushika mimba kwa wakati wanaotaka. Kama kamati, tunataka wanajeshi wetu wafanyiwe vipimo sahihi vya ujauzito wanapotumwa kwa shughuli za kulinda amani,” alisema Mananiso.
Aliongeza: “Hili lifanyike ili kuhakikisha kuwa wanapata matunzo mazuri wakati na baada ya ujauzito. Tunajisikia fahari na wanajeshi wetu hasa katika shughuli ya ulinzi wa amani huko DRC.”
Siku ya Jumatatu, Jeshi la Ulinzi la Afrika Kusini (SANDF) lilitangaza hatua ya kuwarejesha nyumbani askari majeruhi, pamoja na askari wawili waliopata ujauzito.
Wanajeshi hao walikuwa sehemu ya Jeshi la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) walioko nchini DRC.
Hali kadhalika, Mananiso amevitaka vyombo vya habari kuheshimu mipaka na kuwapa nafasi ya kupona majeruhi hao.