Usitishaji vita wa saa 72 umekubaliwa na pande zinazohusika katika mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na unaungwa mkono na DRC na Rwanda, Ikulu ya Marekani ilisema Jumatatu.
"Serikali ya Marekani itatumia kijasusi na rasilimali zake za kidiplomasia kufuatilia shughuli za vikosi vya kijeshi na makundi yenye silaha yasiyo ya serikali wakati wa usitishaji mapigano," msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la White House Adrienne Watson alisema.
Vikosi vyenye silaha na vikundi visivyo vya serikali vilisimamisha mapigano ili kuruhusu kuondolewa kwa vikosi vinavyokalia Mushaki na barabara ya RP1030, kuanzia Jumatatu saa sita mchana kwa Saa za Afrika ya Kati (1000 GMT), Watson alisema katika taarifa.
Kwa mujibu wa shirika la Reuters, hakukuwa na majibu kutoka serikali za Rwanda wala DRC kuhusiana na hilo.
Hapo awali Marekani ilizitaka DRC na Rwanda kupunguza hali ya wasiwasi huku kukiwa na hali mbaya zaidi ya kibinadamu kwenye mpaka kati ya nchi hizo mbili.
Serikali ya DRC inajiandaa kwa uchaguzi mwezi Disemba, huku usalama ukiwa suala kuu kwenye ajenda ya wahusika wote.
Mashariki mwa DRC imekuwa na tatizo sugu la makundi ya waasi zaidi ya mia. Serikali nyingi zilizotangulia na hata iloyoko madarakani sasa zimelaumiwa kushindwa kudhibiti makundi hayo.
Ukosefu huu wa usalama umesababisha baadhi ya maeneo Mashariki mwa nchi kufutiwa upigaji kura, ikiwemo Masisi na Rutshuru.