Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaanza kampeni ya uchaguzi ya mwezi mzima siku ya Jumatatu, huku wagombea 26 wakiwania urais huku kukiwa na hali ya wasiwasi ya kisiasa na mapigano katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Takriban wapiga kura milioni 44 waliojiandikisha, kati ya wakazi karibu milioni 100, watamchagua rais mnamo Desemba 20.
Pia watachagua kati ya makumi ya maelfu ya wagombeaji wa mabaraza ya ubunge na mitaa nchini yenye rasilimali nyingi lakini migogoro na ufisadi uliokithiri.
"Kampeni ya mwanzo-mwanzo" imekuwa ikiendelea kwa muda, huku Rais Felix Tshisekedi, ambaye anawania muhula wa pili, akihudhuria hafla nyingi za umma huku washirika wake wakisifia rekodi yake.
Kampeni rasmi
Kwa uzinduzi wa kampeni rasmi, mikutano mikubwa, mahojiano na vyombo vya habari, mabango makubwa na vipeperushi vya kusambaza vitaruhusiwa.
Siku ya ufunguzi, Tshisekedi atafanya mkutano katika uwanja wa Martyrs huko Kinshasa huku mmoja wa wapinzani wake wakuu, Martin Fayulu, akihutubia mkutano katika mkoa wa karibu.
Kwa jumla kuna rekodi ya wagombea 25,832 wa uchaguzi wa wabunge, 44,110 wa majimbo na 31,234 wa mabaraza ya manispaa, kulingana na Tume ya Uchaguzi (Ceni), ambayo inakabiliwa na mapambano ya kuandaa upigaji kura katika eneo la kilomita za mraba milioni 2.3 na miundombinu chache.
"Kuna dhamira ya kisiasa ya kushikamana na kalenda ya uchaguzi, lakini kuna mashaka juu ya uwezekano wa kiutekelezaji" Tresor Kibangula, mchambuzi wa kisiasa katika taasisi ya utafiti ya Ebuteli, alisema.
Tishio la M23
Maeneo ya mashariki ya nchi hiyo yamekumbwa na mapigano kwa miongo mitatu, na ghasia zinaongezeka tena baada ya kundi la M23, hivi karibuni kuteka sehemu kubwa ya jimbo la Kivu Kaskazini.
Mapigano hayo yatazuia upigaji kura wa kawaida katika maeneo mawili katika jimbo hilo, lakini mchakato mzima utatishiwa iwapo waasi watauchukua mji mkuu wa jimbo hilo Goma.
"M23 haitaichukua Goma," alisisitiza Tshisekedi, ambaye anasema kurejea kwa utulivu ndio kipaumbele chake, pamoja na kuboresha huduma na uchumi, kujenga barabara na kuheshimu uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari.
Rekodi yake ni mchanganyiko, kulingana na wachambuzi, na mbaya kulingana na upinzani, ambayo tayari inaonya juu ya udanganyifu mkubwa.
Mzunguko mmoja wa kupiga kura
Mbali na Fayulu, anayedai kuporwa ushindi mwaka wa 2018, wagombea wakuu wa upinzani ni Moise Katumbi, aliyekuwa gavana wa eneo la madini la Katanga; Daktari Denis Mukwege, ambaye alipokea Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 2018 kwa kazi yake na waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia; na mawaziri wakuu wawili wa zamani.
Rais aliye madarakani anapendelewa kushinda, hasa kwa vile kuna duru moja tu ya upigaji kura, lakini wawakilishi wa makundi matano ya upinzani walikutana wiki hii nchini Afrika Kusini kujadiliana uwezekano wa kupendekeza mgombea mmoja.
Muungano umeundwa na jukwaa la pamoja limepitishwa, lakini Fayulu bado hajajiunga nao.
Wapiga kura wamechanganyika kuhusu faida ya kushiriki kura.
'Kunipotezea muda'
Eunice, mwanafunzi wa jiografia mwenye umri wa miaka 20, anasema "anafuraha" kupiga kura kwa mara ya kwanza.
Ezechiel, mwenye umri wa miaka 24 anayesomea usimamizi wa IT, amevunjika moyo. "Kutakuwa na udanganyifu, kama mwaka wa 2018," alisema. "Sitapoteza wakati wangu."