Ramadhan Kibunga
TRT Afrika, Bujumbura, Burundi
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 68 ameiweka nongwa rohoni na Fayulu yuko tayari kwa 'ulipizaji kisasi' baada ya kushindwa kwenye uchaguzi uliopita wa 2018.
Martin Fayulu dhana yake iko pale pale. Katika kipindi chote cha miaka mitano hadi leo bado anaamini kwamba yeye ndiye alikuwa mshindi halali wa uchaguzi wa mwaka 2018 lakini akafanyiwa 'hila' na ushindi wake kupewa Tshisekedi.
''Nilifanyiwa uhaini mwaka 2018 na Tume ya Uchaguzi CENI pamoja na Korti ya Katiba. Taasisi hizi zilininyima ushindi wangu wa dhahiri kwa faida ya Tshisekedi,'' anadai Fayulu. Hata hivyo, Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo imesisitiza kwamba, matokeo yaliyotangazwa yalikuwa ni halali.
Fayulu ametembelea muda mrefu kwenye kauli mbiu : ''Nataka ukweli kuhusu kura ''
Lakini pengine sasa hayo yamepita. Fayulu anajaribu kuachana na nongwa hizo za kisiasa na kuganga yajayo na hivyo kutafuta nyenzo mpya ili kusonga mbele na pengine kushinda uchaguzi wa urais wa tarehe 20 mwezi huu.
Mkongwe katika sekta binafsi
Martin Fayulu alizaliwa mjini Kinshasa tarehe 21 Novemba mwaka 1957. Licha ya Fayulu kuzaliwa Kinshasa, lakini wazazi wake wana asili ya mkoa wa Kwilu eneo la Bandundu, Magharibi mwa Congo.
Bwana Fayulu amemuoa Esther Ndengue Fayulu na wamezawadiwa watoto watatu.
Sehemu kubwa ya elimu yake aliipokea nchini Ufaransa na Marekani.
Anamiliki shahada mbili kwenye fani ya Uchumi. Kwanza shahada ya Uhasibu katika Chuo Kikuu cha Paris, Ufaransa, kisha shahada ya Utawala na Biashara katika Chuo Kikuu cha San Francisco nchini Marekani.
Martin Fayulu alijijengea umaarufu mkubwa katika uwanja wa Biashara.
Afisa huyo mwandamizi wa zamani wa Kampuni ya Exxon Mobil alihudumu karibu miongo miwili kwenye kampuni hiyo ya petrol ya Marekani na kushikilia nyadhifa muhimu za kimkakati katika uongozi kuanzia Marekani, Ufaransa, Nigeria na Mali. Wadhifa wake wa mwisho ulikuwa kuliongoza Shirika hilo nchini Ethiopia.
Aidha Bwana Fayulu amewekeza nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika katika sekta ya hoteli, makazi na kilimo.
Hatua za Kisiasa
Azma yake ya kujiunga na siasa ilianza mwaka 1991 aliposhiriki katika Mkutano Mkuu wa Kitaifa uliowaleta pamoja wadau wote wa siasa za Congo ili kulazimisha sera ya demokrasia ya vyama vingi.
Wakati huo nchi ilikuwa inaongozwa na rais Mubutu Sese Seko chini ya utawala wa chama kimoja.
Mwaka 2009, Martin Fayulu aliunda chama chake cha ECIDE(Engagement pour la Citoyenneté et le Developpement) yenye maana 'Azma ya Uraia na Maendeleo na kuchukua uongozi wa chama hicho.
'Askari wa wananchi'
Kauli zake nzito za kisiasa zilifanya Fayulu kuvutia sehemu kubwa ya vijana ambao wangependa kuona mageuzi ya kisiasa DRC. Alichaguliwa mbunge wa mkoa kati ya 2006-2011 kisha mbunge wa kitaifa kati ya 2011-2018.
Wakati wa maandamano ya kutetea Demokrasia kati 2016 na 2017, Fayulu alikuwa kwenye safu ya mbele na hata kukoswa risasi ya kichwani wakati wa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji.
Kufuatia tuko hilo, wafuasi wake walimpa jina la 'Askari wa raia.''
Wakongomani wanamuita 'Askari wa wananchi.'
"Hii ni dalili tosha ya jinsi raia wanavyoniunga mkono. Wanaamini mimi ndiye mtu sahihi kuiongoza DRC,'' alinadi Fayulu mbele ya umma mjini Goma.
Mwaharakati wa asasi za kiraia 'Voix du Peuple' Jean Pierre Ilunga amefuatilia sana safari ya kisiasa ya Fayulu. ''Ni kiongozi anayeamini kile anachokitetea, amefunguka kimawazo na ni mtu wa karibu na wafuasi wake, lakini shida yake kubwa ni kufikiria kwamba kila kitu kinawezekana kama anavyotaka yeye, na hapo ndipo anaonekana kwa macho ya wengi kama ni mtu wa msimamo mkali,'' anasema Ilunga.
Awali Martin Fayulu alisusia uchaguzi huu na kuwazuia wafuasi wake kujiorodhesha kwenye ubunge na udiwani kwa madai kwamba kuna ''udanganyifu mkubwa ndani ya daftari la wapigakura.'' Lakini baadae aliwashangaza wengi kwa kuamua kusimama kwenye uchaguzi wa urais.
Albert Ntumba, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Bukavu katika taaluma za siasa anatilia shaka mafaanikio ya Fayulu: ''Uamuzi wake wa awali unaweza kumgharimu kwenye uchaguzi huu kwa sababu tofauti na hali ya mwaka wa 2018, mara hii Fayulu hakuungwa mkono na wagombea wengine. Isitoshe, hata akishinda, atatawala vipi bila wabunge na madiwani?'' alihoji Ntumba.
Mtoto wa mjini ''Vrai Kinoi''
Hata hivyo Fayulu mzaliwa wa mtaa maarufu wa N'djili amejenga imani kubwa ya kukusanya kura katika ngome yake ambayo ni jiji la Kinshasa pamoja na maeneo ya Magharibi mwa Congo hasa jimbo la zamani la Bandundu kwenye asili ya wazazi wake. ''Bahati yangu ni kubwa. Mimi ndiye mpinzani wa kweli. Asieweza kulambishwa mlungula,'' amesikika akijigamba.
Hoja za kampeni
Fayulu amekariri tena azma yake ya mabadiliko ya kina na maendeleo ya nchi. Kiongozi huyo wa chama cha ECIDE ametangaza tayari mkakati wake wa ulinzi na kumaliza tatizo sugu la usalama Mashariki mwa Congo.
''Tutaunda jeshi la nguvu lenye vikosi laki tano na kuwapa mafunzo na vifaa. Tutaweka kambi kubwa za kijeshi Mashariki mwa Congo. Hivyo tutawaeleza wazi wazi Paul Kagame na Yoweri Museveni kwamba Congo sio nchi ya kutekwa au kuchukuliwa hovyo hovyo tu.''
Mbali na ahadi za mkakati wa kudumisha hali ya usalama, Bwana Fayulu amezungukia kwenye kampeni yake katika masuala ya uchumi, elimu na huduma za afya. Aliahidi kupambana dhidi ya ufisadi na kuimarisha uwekezaji katika nyanja muhimu ili kuruhusu ukuaji wa uchumi na ajira katika nchi hiyo.
Amepania pia kubadili mikataba ya madini na ya petroli kwa faida ya nchi. Anasema kazi yake katika shirika kubwa kama Exxon Mobil ilimuandaa kwenye uadhifa huo.