Tume ya Uchaguzi ya Taifa DRC-CENI imesema licha ya changamoto, lakini uchaguzi ufanyika kama ulivyopangwa. Picha/TRT Afrika. 

Licha ya taarifa zinazoenezwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuhusu uwezekano wa kuakhirisha kwa uchaguzi mkuu nchini DRC, Tume Huru ya Uchaguzi CENI imesalia kwenye msimamo wake wa awali na kukiri kwamba itaheshimu muda wa uchaguzi kama ilivyo katika katiba.

CENI inasema ''Itajilazimisha'' kuandaa uchaguzi huo tarehe 20 Disemba licha ya kukabiliwa na ratiba iliyobana na changamoto za kiufundi na vifaa.

Hivyo serikali imeomba msaada wa ziada wa Monusco, Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Congo pamoja na msaada wa ndege kutoka Angola. Ingawa Angola mpaka sasa haijajibu ombi la kutoa msaada wa ndege zake kusaidia katika uchaguzi huo.

Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijatoa jibu kuhusu maombi rasmi ya serikali ya DRC ya kuomba msaada wa ziada wa kiufundi na vifaa katika uchaguzi. Isitoshe mkutano ujao wa Baraza la Usalama umepangwa kufanyika tarehe 20 Disemba, siku ya uchaguzi, siku ambayo kimsingi litajadiliwa azimio jipya la kuongeza muhula wa Monusco.

Tume ya Uchaguzi inataka Monusco kusaidia kupeleka vifaa vya uchaguzi katika maeneo yenye shida za kimiundombinu ya barabara hususan katika mkoa wa msituni wa Équateur.

Hivi karibuni Tume ya Uchaguzi iliomba serikali waweze kupata ndege 4 aina ya Antonov na Helcopter 10 ili kutekeleza vyema majukumu yake.

Licha ya hali hiyo, Tume ya Uchaguzi imeendelea na maandalizi bila kufikiria kuakhirisha ratiba ya uchaguzi.

Kwa matatizo yote hayo, Tume ya CENI inasema imejipanga pia kwa suluhu za mbadala.

Denis Kadima, Mwenyekiti wa Tume hiyo amekariri tena Alhamisi azma hiyo mbele ya wajumbe wa Baraza la Taifa na kuthibitisha kuwa uchaguzi utafanyika tarehe 20 Disemba.

Aidha, kiongozi huyo wa Tume ya Uchaguzi amewachagiza wagombea kuendelea kampeni kwa njia ya amani.

Katika taarifa rasmi, Tume huru ya Uchaguzi CENI imewatolea wito raia kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo. CENI inasema vituo vya kura vitafunguliwa na kufanya kazi kuanzia saa 12 ya asubuhi hadi saa 11 ya jioni, majira ya Congo.

Aidha, wapiga kura ambao tayari waliorodheshwa vizuri na wale ambao kadi zao za kura zina tatizo la kusomeka vizuri au zilipotea, wametakiwa kwenda kwenye vituo vya kura ambapo watachunguzwa na kuhudumiwa na makarani wa uchaguzi kulingana na mahitaji ya kila mmoja.

TRT Afrika