Uchaguzi DRC

Wagombea Urais DRC wameelekeza kampeni zao Mashariki ya DR Congo kuelekea uchaguzi,kwa shamra shamra licha ya suala la usalama kusalia kuwa tete.

Umati wa watu unawasili na kuondoka kati ya viwanja vya ndege vya mkoa huo na vituo vya jiji ili kuwasikiliza wagombea wakizungumza katika viwanja vikuu vya kampeni.

Mbali na kupiga kura y akumchagua rais, raia milioni 44 kati ya idadi ya watu milioni mia moja watapiga kura kuwachagua wabunge wa kitaifa na mkoa na washauri wa mitaa.

Mfanyabiashara na mpinzani maarufu mwenye matumaini Moise Katumbi, mmoja wa watu 23 wanaowania urais alikuwa wa kwanza kwenda Goma, mji mkuu katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Moise Katumbi Mfanyabiashara na mpinzani maarufu mwenye matumaini kwenye uchaguzi wa urais DRC. Picha: Reuters

Katumbi amekosoa majaribio ya rais Felix Tshisekedi ya kukabiliana na uasi wa miaka miwili na harakati ya M23, ambayo inadhibiti maeneo makubwa ya eneo la Kivu Kaskazini.

Tshisekedi, ambaye anasaka muhula mwingine wa miaka mitano, naye alielekea Mashariki, akitembelea eneo la Bunia katika jimbo jirani la Ituri siku ya Jumanne akifuatana na mkewe, Denise Nyakeru Tshisekedi.

"Mniamini tena. Nipeni mamlaka ya pili ili kutekeleza miradi yetu mbalimbali, " alihimiza kwenye hotuba yake katika uwanja wa jiji.

Rais wa DRC Felix Tshisekedi na mkewe, Denise Nyakeru Tshisekedi kwenye kampeni. Picha: AFP 

Daktari bingwa wa maradhi ya kike, na mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel Denis Mukwege naye amezindua kampeni yake ya urais siku ya Jumapili katika mji wake wa nyumbani wa Bukavu, ulioko mkoa wa Kivu Kusini.

Mukwege, muanzilishi wa hospitali na wakfu wa Panzi Mashariki mwa DRC, alishinda tuzo hiyo baada ya kushuhudia majeruhi na magonjwa ya kutisha yaliyowapata waathirika wa ubakaji. Kutoka Bukavu aliendelea na kampeni Butembo na Beni.

Daktari wa maradhi ya kike, na mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel Denis Mukwege naye amezindua kampeni yake ya urais. Picha: Getty

"Mimi ni mgombea wa amani... Kwa pamoja, tumalize njaa na maovu, " Mukwege alisema Mjini Beni, ngome ya wanamgambo wa Allied Democratic Forces wanaohusishwa na Kundi la DAESH.

Martin Fayulu, mgombea mwingine ambaye anazidi kusisitiza kwamba alinyimwa ushindi wake katika kinyang'anyiro cha urais mwaka 2018, yuko tena kwenye kampeni ya urais.

Mgombe wa Urais Martin Fayulu, ambaye pia aliwania kiti hicho 2018. Picha: Reuters

Naye pia alikuwa Beni Jumanne wiki iliyopita, akifuatana na mwanamuziki, na kuwahimiza wapiga kura "kumfungia barabara" Tshisekedi.

"Mkinipigia kura (kwangu), tutaipa Beni kambi ya kijeshi ili Rwanda na Uganda zituheshimu," alisema, katika mji ambao wakaazi hawakupiga kura miaka mitano iliyopita kwa sababu ya janga la Ebola.

Mvutano huo umeathiriwa na kifo cha mwanachama wa Chama cha Katumbi katika mgogoro na wafuasi wa chama cha Tshisekedi.

Raia hao wanatarajia wagombea wa ofisi ya juu zaidi nchini "kurejesha usalama".

AFP