Rais wa DRC Felex Tshisekedi ambae anawania muhula wa pili katika Uchaguzi Mkuu wa Disemba ameahidi kulikomboa eneo lote la Mashariki mwa nchi na kuliangamiza kundi la M23. Picha/ Benjamin Kasembe.

Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Bujumbura, Burundi

Akiwa katika kampeni mjini Goma, rais Felix Tshisekedi ambae anagombea nafasi hiyo kwa awamu ya pili, ameahidi kulikomboa eneo lote la Mashariki mwa DRC na kuliangamiza kundi la M23.

Akiendelea na kampeni ya uchaguzi, Tshisekedi alizuru mji wa Goma mwishoni mwa juma, na baada kuendelea na kampeni yake Kivu Kaskazini katika mji wa Beni.

Licha ya mvua kali, lakini umati mkubwa wa wafuasi wa chama chake waliingia katika uwanja wa Afya mjini Goma wakivalia sare nyeupe huku eneo hilo likiwa chini ya ulinzi mkali.

Bi Thérèse Kasongo ambae ni mkazi wa Kivu Kaskazini ni miongoni mwa waliofika mapema uwanjani hapo akiwa na shauku kubwa ya kusikia mgombea huyo akinadi sera zake. ''Sina mahitaji mengi naitaka amani. Ikiwa tutapata amani, amani ndio kila kitu. Hiki ndio kilio chetu cha mda mrefu. Na tuna imani naye,'' amesema Therese.

Ni katika eneo hilo, ambapo kumekuwa na mapigano yanayoendelea ambayo yanahusisha vikosi vya serikali na waasi wa M23.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Pierre Kongolo matumaini yake makubwa ni kuona uasi huo unamalizika haraka iwezekanavyo. ''Ni miaka mitano yuko mamlakani, tuna matumaini kwamba iwapo atapewa muhula wa pili, atafanya vizuri na kukomesha vita. Ameonyesha kuwa ni mpambanaji. Tumpe tena kura,'' anasema Pierre.

''Nadhani sehemu kubwa ya sera yake sawa na watetezi wengine ni porojo tu za uchaguzi kutafuta kura. Tukumbuke yuko madarakani sasa ni miaka mitano. Lakini ameshindwa hata kutembelea maeneo mengi ya Mashariki mwa Congo, lakini leo anakuja kutafuta kura. Ninaamini kufikia maendeleo hayo itakuwa ni vigumu kama hakutakuwa na amani na utulivu katika eneo hili.''

Albert Ntumba, mhadhiri Chuo Kikuu

Akiingia jukwani, Felix Tshisekedi alimlaumu jirani yake kiongozi wa Rwanda Paul Kagame kuwa chanzo cha usalama mdogo na kuahidi kurejesha amani na usalama katika eneo hilo.

''Hakuna kikubwa kilichosalia ili kumshinda kikamilifu adui. Mniamini. Hivi karibuni nitawapa ushindi kamili kwa kulikomboa eneo lote la Mashariki mwa Congo,'' alinadi Rais Felix Tshisekedi.

Rais wa DRC akiwapungia mkono wafuasi wake katika moja ya kampeni zake za urais.  Picha/ Benjamin Kasembe.

Kwa upande wake, Rwanda imejibu tuhuma hizo mwishoni mwa juma na kusema ni, ''Kitisho na uchochezi wenye lengo la kukwepa kukabiliana na hali halisi baada ya mtawala wa DRC kushindwa katika masuala ya usalama na utawala.''

Akiwa bado jukwaani mjini Bukavu, Felix Tshisekedi pia alitumia fursa hiyo kunadi mafanikio yake ya miaka mitano.

"Tulipofika mamlakani, akiba ya nchi ilikuwa milioni 840, leo akiba hiyo imefikia dola bilioni 5. Bajeti ya nchi ilikuwa inazungukia kwenye dola bilioni 5. Hivi leo tumefikia kwenye dola bilioni16. Ikiwa mtanipa muhula wa pili, nitautumia kuendelea kubuni mipango yamaendeleo,'' amesema Tshisekedi.

Moïse Katumbi mgombea mkuu wa upinzani DRC akiwa katika kampeni.  Picha/ Benjamin Kasembe.

Rais Tshisekedi pia alikwenda katika mji wa Uvira na Fizi kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika ambapo alitilia mkazo sera ya kijamii na kuahidi elimu ya bure ya sekondari.

''Tayari wanafunzi wanasoma bure katika shule za msingi, ikiwa mtanichagua, nitafanya shule ya sekondari kuwa bure na kuimarisha huduma za afya.

Ahadi hiyo ya mgombea huyo wa urais ilionekana kumgusa Jeanne Furaha wa mjini Uvira. ''Kwa kweli nitamchagua 'FATCHI' leo tu mtoto wangu amefukuzwa shule kwa vile sijalipa karo za shule sasa ni miezi miwili. Hii kero inakwenda kumalizika.''

Lakini wadadisi wa siasa wamekuwa na shaka kutokana na baadhi ya ahadi zinazotolewa. Albert Ntumba, ambae ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha ISP mjini Bukavu, anasema, ''Nadhani sehemu kubwa ya sera yake sawa na watetezi wengine ni porojo tu za uchaguzi kutafuta kura. Tukumbuke yuko madarakani sasa ni miaka mitano. Lakini ameshindwa hata kutembelea maeneo mengi ya Mashariki mwa Congo, lakini leo anakuja kutafuta kura. Ninaamini kufikia maendeleo hayo itakuwa ni vigumu kama hakutakuwa na amani na utulivu katika eneo hili.''

Uchaguzi Mkuu wa DRC unatarajiwa kufanyika Disemba, 20, 2023.  Picha/ Benjamin Kasembe.

Wakati huo huo, mpinzani mkuu Moïse Katumbi yeye alikuwa mjini Kinshassa Jumamosi. Aliahidi kuifanya Kinshassa kuwa mji mzuri wa Afrika na kuupa miundombinu ya kisasa. Aidha, Katumbi aliahidi kupunguza gharama za maisha huku akiwataka wafuasi wake wasiondoke kwenye vituo vya kupiga kura kabla ya kuchapishwa matokeo ili kuepuka kile alichokiita, ''udanganyifu na wizi wa kura uliopangwa.''

Uchaguzi mkuu wa tarehe 20 Disemba utawahusisha wagombea wa urais wasiopungua 21. Lakini mdadisi wa siasa za maziwa makuu Dk Jumanne Abdoul anasema mchujo umeanza kuonekana '' Baada ya kampeni za wiki tatu, inaonekana wazi kwamba mchuano mkali utakuwa kati Tshisekedi na Katumbi. Na inawezekana baadhi ya wagombea wiki hii wakaungana na upande mmoja na mwengine na hapo tunaweza kuanza kuona vizuri sura ya uchaguzi.''

TRT Afrika