Moise Katumbi, ni mfanyabiashara maarufu nchini DRC, lakini pia ni mwanasiasa anaewania nafasi ya urais wa nchi hiyo. 

Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Bujumbura, Burundi

Mfanyabiashara tajiri, mmiliki wa klabu maarufu ya soka na kiongozi wa Kisiasa mwenye shauku ya kuwa rais wa nchi; Moïse Katumbi Chapwe Soriano mwenye umri wa miaka 58 alizaliwa katika eneo la Kashobwe katika jimbo la Katanga.

Baba yake Moïse ni Nissim Soriano, mwenye asili ya Ugiriki aliyehamia Congo katikati mwa Vita vya Dunia baada ya kukimbia Rhodes na hivyo kuchukua hifadhi katika eneo la Kashobwe, karibu na Ziwa mpakani na Zambia ambako alizindua biashara ya samaki. Na hapo ndipo alipozaliwa Moïse Katumbi tarehe 28 Disemba mwaka 1964. Mama yake Moïse ni Virginie Mwende mzaliwa wa Congo.

Safari yake ya maisha inaashiria kama mtu mpambanaji lakini mwenye maono ya kufikia pale anapopalenga. ''Nilitumika sana katika maisha yangu. Ningependa kwenda Chuo Kikuu, lakini biashara ilinishawishi zaidi sana katika maisha yangu,'' anasema.

Moise Katumbi, tangu mwaka 1997, alichukua uongozi wa timu maarufu barani Afrika ya kandanda ya 'Tout Puissant Mazembe' klabu yenye historia na yenye ngome yake katika mji wa Lubumbashi.

Anatembea maeneo mengi nchini mwake na hata ugenini akiwa na ndege yake binafsi, lakini hilo haimzuii mara nyingi kupiga picha akiwa kwenye matembezi ya miguu au kwenye baskeli yake katikati ya umma.

Kawaida Moïse huvaa sana kofia zenye mitindo tofauti na licha ya umri wake, bado ameendelea kuwa mtanashati na 'mwanamitindo kwenye mavazi katika nchi inayosifika kwa mavazi.

"Anafanya kampeni yake kama anavyofanya biashara bila kupuuzia chochote. '' Alipata muda wa kujiandaa na kutengeneza vizuri mipango yake ya kampeni," anasema Yves Kasongo kutoka Lubumbashi, DRC.

Katika uchaguzi wa urais, mwaka wa 2018, Moïse Katumbi hakuweza kusimama kutokana na tuhuma za kuhodhi ardhi na kumiliki 'mamluki' na hivyo kuhukumiwa hadi kulazimika kuitoroka nchi.

Moise Katumbi, mwaka 2018, alilazimika kumuunga mkono Martin Fayulu katika uchaguzi uliopita. Picha/Mseke Dide.

Hali hiyo ilitokana na kuachana mikono na mshirika wake wa zamani Joseph Kabila hadi kulazimika kuitoroka nchi.

Katumbi alilazimika kumuunga mkono Martin Fayulu katika uchaguzi wa mwaka 2018 lakini kutokana na matokeo ya Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo, Fayulu aliangushwa kwenye uchaguzi huo na Tchisekedi, ambae hivi sasa ndiye aliyeshika hatamu.

Katumbi alirudi Congo baada ya Rais Felix Tchisekedi kutawazwa kuwa Rais mwaka 2019.

'Nchi yangu'

Baada ya Shule ya Sekondani, Moïse Katumbi alianza safari yake ya ujasiriamali katika uvuvi 'kazi ya Baba' akiwa pia wakati huo huo mteja mkubwa wa Kampuni ya umma ya madini ya Gecamine.

Sambamba na hilo, aliendeleza kutengeneza bidhaa mbalimbali katika kampuni yake ya kilimo lakini pia akiwekeza zaidi katika uchukuzi, huduma za madini ya shaba na cobalt. Katumbi alisema, ''Nalima kwenye eneo la hekari 6000 za mahindi na hekari 500 za soja.''

''Wanadanganya. Mimi ni Mkongomani, na hii nchi, ni nchi yangu.''

Moise Katumbi, mgombea urais nchini DRC

Mwaka 1997, alianzisha kampuni ya madini ya 'Mining Company Katanga (MCK) na baadae 2015 akaiuza kwa Kampuni ya Necotrans ya Ufaransa.

Utajiri wake haujulikani rasmi. Lakini kabla ya kuwa Gavana wa jimbo la Katanga, alikiri kuwa Kampuni yake ilikuwa na mtaji wa dola millioni 400 katika mwaka wa 2007. Uwekezaji wake zaidi umejikita pia katika biashara ya simenti na ngano. Wadadisi wa siasa za Congo wanasema utajiri wake mkubwa unaweza kuwa moja kwa vichocheo muhimu katika uchaguzi huu wa urais wa Disemba 20.

Shabiki mkubwa wa Kandanda

Tangu mwaka 1997, Moïse Katumbi alichukua uongozi wa timu maarufu barani Afrika ya kandanda ya 'Tout Puissant Mazembe' klabu yenye historia na yenye ngome yake katika mji wa Lubumbashi.

Timu inayofahamika kwa kila utani, ''Les Corbeaux'' au 'Kunguru Weusi' iliundwa mwaka 1939 Na tayari imetwaa vikombe 5 vya ubingwa wa Bara ikiwemo mataji matatu ya ligi ya mabingwa Afrika (2009,2010,2015) chini ya uongozi wa Moïse Katumbi.

Moise Katumbi akiwa katika moja wapo ya kampeni zake nchini DRC kuelekea uchaguzi mkuu Disemba, 20.

Alijitolea kuwekeza ndani ya klabu hiyo na kuipa uwanja wa kisasa wa Kamalondo wenye uwezo wa kuwachukua watu elfu18 na umekidhi vigezo vya kimataifa. Lakini pia aliunda kituo cha mafunzo ya soka kwa vijana ''Katumbi Football Academy.''

Katumbi ana mke, ambae ni Bi Carine Nahayo Katumbi mzaliwa wa Bujumbura,Burundi.

Wamewapata watoto sita ambao ni, Nissim, Champion, Lael, Moses, Ishmael na Jonathan. Katumbi ni muamini wa dhehebu la Katolika.

Moja ya burudani zake anazopenda ni kucheza mara kwa mara mchezo wa tenisi. Moïse Katumbi alisema hapendi siasa kutokana na 'porojo' zake na kujawa na uongo mwingi. Hata hivyo, baadae alionekana kubadilisha msimamo na mwaka 2007 aliingia katika siasa na kuchaguliwa Gavana wa Mkoa tajiri wa madini wa Katanga ambao aliouongoza hadi mwaka 2015.

Moïse Katumbi anafahamika sana kama 'Mtu wa Watu' lakini baadhi ya watu hasa wakosoaji wake wanamuona kama mtu mwenye kutaka sifa na umaarufu pamoja na kuzungukwa na wapambe.

Aidha wakosoaji wake wanamtuhumu kwamba alitumia nafasi yake ya Gavana kwa kujitajirisha. Ingawa binafsi kila mara amekuwa anakana tuhuma hizo, kwa kuseam, ''Nilijenga barabara, hospitali, shule. Kama nisingefanya hivyo siningekuwa maarufu. Jina hutengenezwa. Lazima binaadamu abaki hai hata baada ya kifo chake. ''

Hata hivyo, umaarufu wake, hauko katika eneo la Katanga na mji wake wa Lubumbashi tu, lakini pia kwenye maeneo mengine ya DRC. Wakati huo huo, kwa sababu mcheza kwao hutunzwa, watu ''wake'' hasa kutoka Lubumbashi wanamuona kama ni ''Zawadi ya Mungu kwao '' au ''Chaguo la Mungu.''

Kiongozi huyo wa chama cha "Ensemble pour la République (Pamoja kwa Ajili ya Jamhuri) anaungwa mkono kwenye uchaguzi wa urais na viongozi wengine wanne ambao wameachia ngazi kwa niaba yake. Ambao ni pamoja na waziri mkuu wa zamani bwana Augustin Matata Ponyo, Frank Diongo kutoka chama cha mrengo wa Lumumba, Kijana mfanyabiashara Seth Kikuni Masudi pamoja Delly Sesanga.

Mfanyabiashara na mwanasiasa Moise Katumbi ni miongoni mwa wagombeaji wakuu katika kinyang'anyiro cha urais 2023. Picha: Reuters

''Katumbi anafahamu vyema kwamba hapendwi Kinshassa na maeneo ya magharibi, nadhani alifanya vizuri kuungana na watetezi wengine,'' anasema mhadhiri wa Chyuo Kikuu Jean Marie Katubadi.

Muungano huo unafanya Moïse Katumbi kuwa miongoni mwa wapinzani wakubwa wa Felix Tshisekedi.

Baadhi ya wapinzani wake hâta hivyo wanamchukulia kama mgeni ''chotara'' na kueleza wazi wazi kama mama yake pia ana asili ya Zambia. Na kwamba pia, "anatanguliza pesa katika kila kitu."

Lakini Moïse Katumbi mwenyewe, anasema yeye ameweka mbele mafanikio yake katika jimbo la Katanga ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, shule, maendeleo ya kilimo na hivyo kuthibitisha na kuashiria kwamba atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuweza kuiongoza nchi nzima ya DRC.

Tofauti na miaka ya nyuma, mara hii tiketi yake ya kugombea imeorodheshwa na kuidhinishwa na Mahakama ya Katiba. Mahakama hiyo ilitupilia mbali rufaa ya kupinga uraia wake wa Congo. Lakini mjadala huo bado uko mbali kufungwa.

Timu ya mpira yaTP Mazembe imekuwa chini ya ulezi wa Moise Katumbi. 

Ukiacha kuchukuliwa moja kwa moja kama mgeni, wapinzani wake kama Felix Tshisekedi wanamchukulia miongoni mwa wagombea wa ''nchi za kigeni'' na hili wanalitamka wazi kwenye kampeni, kitu ambacho Katumbi Chapwe ameshindwa kuvumilia:

''Wanadanganya'' aliwajibu kwa kusititiza kwenye mkutano wa kampeni, ''Mimi ni Mkongomani, na hii nchi, ni nchi yangu.''

Ilani yake kwenye uchaguzi huu imejikita zaidi kwenye mageuzi ya taasisi, kuinua uchumi hasa kwa kuipa Congo taasisi imara na kupiga vita ufisadi.

Aliahidi iwapo atachaguliwa atabuni ajira zaidi ya milioni 3 na ujenzi wa madarasa elfu 50 pamoja na kutoa ajira za walimu elfu 15 katika nchi nzima huku akiipa Congo barabara kwenye umbali wa kilomita elfu 28 na maji safi kwa raia wote.

TRT Afrika