Misheni ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), inayojulikana kama MONUSCO, imesema imeidhinisha mpango wa kuondoa wanajeshi wake katika taifa hilo la Afrika ya Kati, bila kutoa maelezo kuhusu muda.
Katika taarifa, misheni hiyo ya kulinda amani ilisema imeidhinisha "hati ya kujitoa kwa haraka, kwa hatua, kwa mpangilio na kwa uwajibikaji" kutoka nchini humo.
Hati hiyo ina mpango na ratiba ya kuondoa, lakini misheni hiyo ya kulinda amani haikutoa maelezo mengi isipokuwa kusema itatekelezwa kwa awamu tatu.
MONUSCO ni mojawapo ya misheni kubwa na ghali zaidi ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani, ikiwa na bajeti ya kila mwaka ya takribani dola bilioni moja.
Uepo wao tangu 1999
Walinzi wa amani wamekuwepo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu mwaka 1999 lakini vurugu za wanamgambo zimeendelea kuikumba sehemu ya mashariki ya nchi.
Makundi kadhaa yenye silaha yanafanya shughuli zake mashariki mwa DRC, ambayo ni matokeo ya vita vya kikanda vilivyotokea katika miaka ya 1990 na 2000.
Jeshi la amani la MONUSCO lenye wanajeshi 14,000 kwa sasa halipendwi sana kwa kuonekana kwamba halijafanya vya kutosha kuzuia ghasia.
Serikali ya Kongo imetoa ombi la kuondoka "kwa haraka" kwa MONUSCO.