Katika barua ambayo aliandikia wananchi wake katika akaunti yake ya X rais Yoweri Museveni amesema Uganda imekuwa ikifanya mashambulizi ya anga dhidi ya magaidi wa Allied Democratic Forces (ADF) katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
"Hapa chini ni majina ya watu waliokufa katika shambulio la Septemba 16, 2023. Takriban 200 kati yao walikufa. Tangu wakati huo, mashambulizi mengine yamefanywa," alielezea huku akiandaka orodha ya majina 57 ambayo anasema hana uhakika ikiwa ni majina wa kweli ya magaidi hao.
"Tumekuwa tukifanya mashambulizi ya anga dhidi ya magaidi nchini Congo. Kwa kawaida tunatambua tunaowalenga kwa kutumia njia za teknolojia na binadamu. Kwa kutumia njia hizo, unaweza kujua kwamba magaidi wengi waliuawa," alielezea.
Waasi wa ADF walitoka magharibi mwa Uganda mwishoni mwa miaka ya 1990 kwa nia ya kupindua utawala wa Rais Yoweri Museveni lakini walizidiwa nguvu na jeshi la Uganda.
Walikimbilia msituni Mashariki mwa DRC, ambapo mara nyingi hushambulia vijiji na kuua watu.
Uganda imekilaumu kikundi hicho cha ADF, ambacho ni mfungamano na kundi la Daesh, kwa mauaji na mashambulizi.
Mashambulizi ya hivi majuzi yalikuwa mwezi Oktoba ambapo watalii wawili wa kigeni na raia mmoja wa Uganda waliuawa katika Hifadhi ya Taifa iliyopo magharibi mwa Uganda, na gari lao kuteketezwa kwa moto.
Mwezi Juni mwaka huu kikundi cha ADF kilifanya uvamizi wa usiku wa manane katika shule ya upili ya Lhubirira Secondary huko Mpondwe, Kasese magharibi mwa Uganda.
Eneo hilo lipo mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ripoti zinasema kuwa wanafunzi 42 waliuawa.
Hili lilikuwa shambulio baya zaidi la aina yake kuwahi kutokea nchini Uganda tangu mwaka 2010.
Uganda inasema imeweka usalama katika mipaka yake na DRC kuhakikisha kuwa kikundi cha ADF ambacho kinasemekana hujificha misituni, hakifanya mashambuzi nchini Uganda.