Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani, WFP, linaonya kuwa ufadhili kwa wakimbizi nchini Uganda ni wa chini mno.
Uganda imewapa makazi zaidi ya wakimbizi milioni moja na laki tano kutoka nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan Kusini, Burundi na Somali.
"Mahitaji ya wakimbizi wa Uganda hayatoshi, na kulazimisha WFP kusaidia watu walio hatarini zaidi pekee kwa msaada wa chakula," Shirika hilo limesema.
"Bila uingiliaji wa haraka ili kusaidia kujenga maisha endelevu, salama, na yenye heshima, 82% ya wakimbizi wako katika hatari ya kupata chakula na usalama wa lishe," limeongeza.
Kwa sasa, takriban asilimia 14 ya wakimbizi wanachukuliwa kuwa hatarini sana na wanapata mgao wa chakula kwa asilimia 60.
Asilimia 82 wameainishwa kama walio katika mazingira magumu na wanapokea asilimia 30 ya mgao wa chakula.
Takriban asilimia 4 ya wakimbizi wanachukuliwa kuwa wanajitegemea.
Uganda imewapa makazi wakimbizi milioni moja na laki tano kutoka nchi tofauti.
Sera yake ya wakimbizi inasifiwa sana kwa kuwa jumuishi na inayoendelea, lakini migogoro inayoongezeka duniani imesababisha rasilimali kupungua.
Wataalamu wanasema sambamba na ahadi za kimataifa kama zile zilizowekwa katika Mkataba wa Kampala kushughulikia sababu kuu za watu kuhama - ikiwa ni pamoja na athari za hali ya hewa - na kuwapa wakimbizi msaada wanaohitaji ili kustahimili majanga na kujenga uwezo wa kujitegemea, mwitikio wa wakimbizi utakuwa endelevu tu ikiwa kuna mwelekeo wa kukabiliana na hali ya hewa.
"Hiyo ni lazima iandae wakimbizi na jumuiya zinazowakaribisha kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Ni lazima tuwekeze katika nishati mbadala ili kuhakikisha wakimbizi wanapata mafuta safi yanayohifadhi afya zao na mazingira. Ni muhimu pia kupanda na kukuza utamaduni wa upandaji miti ili kulinda mifumo ya chakula," Shirika la WFP linasema.
Na huku mizozo ikiendelea katika nchi nyengine kama Sudan kuendelea kulazimisha watu kukimbia makazi yao, kuna hofu kuwa usaidizi kwa wakimbizi utapungua zaidi.
"Suluhisho la suala la ongezeko la wakimbizi ni demokrasia na kuunda hali mzuri ya maisha katika kila nchi," Waziiri Mkuu wa Uganda amesema katika mkutano wa wakimbizi Global Refugee Forum unaofanyika Uganda.