Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini Uganda imetahadharisha kuanza kwa mvua za El Nino katika maeneo mbalimbali ya nchi.
"El Nino iliyotabiriwa tangu mwezi Aprili 2023 imefika," Shirika hilo lilisema katika mtandao wake wa X.
Hussen Seid, ambae ni mtaalamu wa Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha IGAD, kinachoitwa ICPAC analezea El Niño kama hali ya ongezeko la joto katika bahari ya Pasifiki ya kati na mashariki.
"Kuwepo kwa El Niño kunaathiri mwelekeo wa hali ya hewa kote ulimwenguni. Tukio jengine la msingi lijulikanalo kama ‘Indian Ocean Dipole’ linaendelea kukuwa katika bahari ya Hindi na kutarajiwa kuzidisha athari na matokeo ya El Nino,” Seid ameongezea.
El Nino ni nini?
Dkt Mafuru Kantamla Biseke, Meneja - Ofisi Kuu ya Utabiri Tanzania, TMA, anaeleza kwamba El Nino ni jina la tukio la hali ya hewa ambalo linaweza kutokea katika Bahari ya Pasifiki ya Kati na kuathiri hali ya hewa duniani kote.
Tukio hili linahusisha joto la juu tofauti na joto la kawaida la bahari katika eneo la Bahari ya Pasifiki ya Kati na linaweza kusababisha athari mbalimbali za hali ya hewa katika maeneo tofauti duniani.
El Nino inaweza kusababisha mvua nyingi na mafuriko katika maeneo ambayo kawaida ni kavu.
Ujumbe wa tahadhari
Mara nyingi El Nino huleta mvua nyingi kupita kiasi na hata madhara katika maeneo ya mabonde kutokana na mafuriko.
"Tunatoa wito kwa madereva wa magari hasa watumiaji wa pikipiki (boda boda) kuwa makini," imeonya Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Uganda.
"Epuka maeneo yanayokumbwa na mafuriko haswa ukiwa unaendesha gari. Pia tahadhari kwa kutokuwa na uwezo wa kuona vizuri unapooendesha gari , egesha mahali salama hadi uweze kuona vizuri," Mamlaka hiyo imeshauri.
Maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Uganda huathiriwa mara kwa mara na maporomoko ya matope kwa sababu ya mvua nyingi.
Kutokea kwa mvua kubwa na mafuriko katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 1997 nchini Uganda kulichangiwa na El Nino na hali inayoitwa 'Dipole ya Bahari ya Hindi' (IOD) kutokea kwa wakati mmoja.
Hatari ya Kiafya
Tayari nchi jirani ya Kenya inajiandaa kwa hali ya El nino.
Miongoni mwa athari za El Nino ambazo zimetajwa na Shirika la Afya Duniani ni pamoja na utapiamlo, kipindupindu, homa, malaria na homa ya chikungunya ambayo inaenezwa na mbu wenye virusi.
Homa ya Chikungunya dalili zake ni pamoja homa na kuhisi kichefuchefu au hali ya kutapika, maumivu ya kichwa, homa kali, kupata maumivu ya viungo hasa miguu an mikoni kuwa na uchovu wa mwili.
Maeneo mengine ya Afrika Mashariki
Hii inakuja wiki moja baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania, TMA, kutoa taarifa kwa TRT Afrika wiki moja iliyopita kuwa El Nino inakuja nchini humo pia.
Dkt Biseke amesema ingawa athari zinatofautiana, lakini amewataka wanachi kujiandaa kwa ajili ya El Nino.
"Kutakuwa na El Nino na mchango wake mkubwa ni kuongeza mvua mwaka huu katika maeneo mengi Tanzania na Afrika Mashariki. Kuepukana na madhara, watu wachukue hatua stahiki na tahadhari jinsi walivyoelekezwa na serikali," alisema Dkt Mafuru.
Mara ya mwisho, ukanda huo wa Afrika Mashariki kukumbwa na janga la El Nino ilikuwa ni mwaka 1997 ambapo kulikuwa na athari mbalimbali ikiwemo, mafuriko yaliyosababisha uharibu wa mashamba na miundombinu pamoja na ukosefu wa chakula.