Somalia imejiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashraiki. Picha/ TRT Afrika 

Somalia imejiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki rasmi katika sherehe iliyofanyika mjini Entebbe nchini Uganda na kuongozwa na mwenyekiti wa EAC rais wa Sudan Kusini Salva Kiir.

"Somalia tayari ni mwanachama wa Jumuiya hii. Nina uhakikika kuwa ukienda Mogadishu sasa hivi utapata bidhaa kutoka Kenya au hata Uganda, kwa hivyo tunachoshuduia leo ni kama tu ubatizo wa uhusiano ambao tayari unaendelea," rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema.

Uanachama wa Somalia ulitangazwa rasmi katika mkutano wa marais wa EAC katika mji wa Arusha, Tanzania mwezi Novemba mwaka huu.

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia ametia saini mkataba huo wa uanachama akisema ni wakati wa kujivunia sana kwa Somalia.

"Jumuiya hii ndipo ambapo Somalia inafaa kuwepo," rais Sheikh amesema.

"Inaashiria kutimizwa kwa matarajio yetu ya pamoja na ni kielelezo cha matumaini ya siku zijazo iliyojaa uwezekano," ameongezea.

"Ujumuishaji wa Somalia utaimarisha muunganisho wa watu, rais wa Somali tayari tupo hapa katika nchi za Afrika Mashariki. Sisi tayari tupo katika familia hii lakini leo kama vile rais Museveni alivyosema ni kama tumezaliwa upya kupitia sherehe hizi kwa madhumuni ya kuweka uhusiano wetu rasmi na halali," rais Sheikh ameongezea.

Somalia sasa inajiunga na Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda katika Jumuiya hiyo.

"Maendeleo dhidi ya Al Shabaab nchini Somalia, kurejesha ardhi kubwa na hatua muhimu za hivi majuzi katika uhusiano wa kimataifa zinaonyesha dhamira yetu na azma yetu ya kuwa mchangiaji mkuu wa ustawi wa eneo hili na ulimwengu kwa ujumla," rais Sheikh ameongezea.

Somalia inasifika kwa kujivunia ukanda mrefu zaidi wa pwani katika bara la Afrika huku ikiwa na zaidi ya kilomita 3,000 (maili 1,800) na uanachama wake ni mlango wa EAC uarabuni.

Ni wanachama wengine wawili pekee - Kenya na Tanzania wenye bahari katika Jumuia.

TRT Afrika