Marekani imetangaza vikwazo vipya vya kupunguza mauzo ya mafuta ya Iran, vikwazo hivi vinalenga meli 14. Haya yanajri muda mfupi tu baada ya nchi nchi hizo mbili kuhitimisha mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja nchini Oman.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Tommy Pigott, alisema siku ya Ijumaa kwamba Iran inatumia mapato ya mafuta yake "kufadhili shughuli za kuleta taharuki duniani na kuongeza ukandamizaji ndani ya Iran."
Pigott alisema katika taarifa: "Rais Donald Trump ameahidi kupunguza mauzo haramu ya mafuta na bidhaa za kemikali zitokanazo na mafuta za utawala wa Iran, katika hatua ya kuishinikiza utawala huu."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema itazuia miamala yoyote na meli 14 zinazodaiwa kutumika kusafirisha mafuta ya Iran.
Pia ilitangaza vikwazo dhidi ya mashirika 15 na watu wawili.
Tangu muhula wa kwanza wa Trump, Marekani imeweka vikwazo kwa lengo la kulazimisha nchi nyingine zote kuto nunua mafuta ya Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikutana kwa njia isiyo ya moja kwa moja na wajumbe wakuu wa Trump kuhusu programu ya nyuklia ya nchi yake huko Oman Ijumaa na alisema kulikuwa na "hali chanya" katika mazungumzo hayo.
Mazungumzo haya yanakuja wakati Iran inakabiliwa na maandamano makubwa tangu Mapinduzi ya 1979.
Trump alikuwa ametishia kutumia nguvu dhidi ya Iran na kuongeza uwepo wa kijeshi wa Marekani karibu na pwani za Iran.













