| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
UAE inaunga mkono hatua ya kijeshi ya kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz
Abu Dhabi inatathmini uwezekano wa kushiriki moja kwa moja huku mataifa makubwa yakitazamia kuunda muungano wa kulinda njia muhimu ya mafuta.
UAE inaunga mkono hatua ya kijeshi ya kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz
Takribani asilimia 20 ya mafuta yote duniani hupitia Mlango wa Hormuz kila siku, hali inayoufanya kuwa mhimili muhimu kwa masoko ya nishati. / / Reuters
tokea masaa 3

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) unajiandaa kuunga mkono juhudi zinazoongozwa na Marekani za kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz kwa kutumia nguvu, mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani.

Kwa mujibu wa ripoti ya The Wall Street Journal iliyochapishwa siku ya Jumanne, ikinukuu maafisa wa nchi za Kiarabu, UAE inashawishi kupitishwa kwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakaloruhusu hatua za kijeshi. Aidha, inaishinikiza Marekani pamoja na washirika wake wa Ulaya na Asia kuunda muungano wa kulinda njia hiyo ya kimkakati ya majini.

Abu Dhabi inatathmini uwezekano wa kushiriki moja kwa moja katika mgogoro huo kwa mara ya kwanza, ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu ya kijeshi kama operesheni za kusafisha mabomu ya baharini, ripoti hiyo ilieleza.

Katika taarifa iliyonukuliwa na gazeti hilo, Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE ilisema kuwa kuna “makubaliano mapana ya kimataifa kwamba uhuru wa urambazaji katika Mlango wa Hormuz lazima ulindwe,” ikionyesha wasiwasi mkubwa wa kimataifa kuhusu usumbufu wa njia hiyo muhimu.

Hatua hii inakuja wakati vita vinavyoendelea kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran vinavyozidisha hali ya sintofahamu katika eneo la Ghuba.

Mvutano umeongezeka tangu Machi 2, baada ya Iran kutangaza vikwazo vya urambazaji katika mlango huo na kuonya kuwa inaweza kulenga meli zinazopita bila uratibu.

Takribani asilimia 20 ya mafuta yote duniani hupitia katika njia hii nyembamba kila siku, hali inayoufanya kuwa mhimili muhimu kwa masoko ya nishati ya kimataifa.

Kuongezeka kwa ukosefu wa usalama tayari kumesababisha kupanda kwa bei ya mafuta, pamoja na gharama za usafirishaji na bima, na kuongeza hofu ya athari kubwa zaidi za kiuchumi iwapo mgogoro huu utaendelea kuongezeka.

CHANZO:TRT World and Agencies