Mashambulizi hayo yanaripotiwa kufanywa na wapiganaji wanaohusishwa na kundi la JNIM, pamoja na wapiganaji wanaotaka kujitenga wa Tuareg.
Katika taarifa hiyo iliyosainiwa Aprili 25, Traoré alisema mashambulizi hayo yalilenga maeneo mbalimbali ndani ya ardhi ya Mali na yalikuwa sehemu ya mkakati mpana wa uchokozi dhidi ya kanda ya Sahel katika juhudi zake za kujipatia uhuru wa kujitawala.
Alibainisha kuwa ukubwa, uratibu, vifaa na silaha zilizotumika katika mashambulizi hayo inadhihirisha wazi kwamba yalipangwa kwa muda mrefu, yakilenga kusababisha vifo vingi miongoni mwa vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na kusambaza hofu kwa raia nchini Mali na katika eneo lote la Sahel.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kuendelea kwa mashambulizi hayo “ya kikatili na yasiyo ya kibinadamu” kunaashiria uwepo wa nguvu zinazopinga juhudi za ukombozi wa Sahel chini ya mfumo wa AES.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilisema malengo ya washambuliaji hatimaye yalizimwa na Jeshi la Mali, ambalo lilifanikiwa kuyazuia mashambulizi hayo.
AES ilisisitiza kuwa mashambulizi hayo hayataathiri azma ya mataifa ya Sahel, ikieleza kwamba wananchi wa eneo hilo wanaendelea kuwa na dhamira ya kuishi kwa uhuru, amani na heshima licha ya changamoto za usalama zinazoendelea.
Muungano huo ulitoa pole kwa familia za waliopoteza maisha na kuwatakia nafuu ya haraka waliojeruhiwa, huku ukionyesha “mshikamano kamili, usio na masharti na wa kindugu” kwa watu wa Mali, serikali yao.
Taarifa hiyo pia ilitoa shukrani kwa nchi washirika na marafiki kwa msaada wao, na kuthibitisha tena dhamira ya shirikisho hilo kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na vitisho vya usalama na kuendeleza juhudi zake za kufikia uhuru wa kujitawala na utulivu katika eneo hilo.
















