Uturuki imeanza kanuni mpya za mitandao ya kijamii yenye lengo la kuongeza ulinzi kwa watoto na vijana wanapotumia mitandao.
Hatua hii inaungana na nchi kama Australia na Ufaransa ambazo zimechukua hatua kama hizo. Kanuni hizo zimejikita katika kuongeza usalama, uwajibikaji wa mitandao na kuhakikisha inachukua hatua za haraka dhidi ya maudhui yenye madhara.
Chini ya sheria mpya, watoto chini ya miaka 15 hawataweza kujisajili katika mitandao ya kijamii, huku makampuni yakitakiwa kuweka mfumo imara wa uthibitisho wa umri.
Watoa huduma pia watatakiwa kutoa huduma tofauti kwa watumiaji chini ya miaka 15 na zaidi.
Utekelezaji wa hatua kwa hatua
Kanuni hizo zimeweka mfumo imara wa usimamizi wa wazazi, ikitaka kuwepo kwa mfumo wenye kuangalia ufunguaji wa akaunti na muda wa kuwa hewani.
Makampuni ya mitandao ya kijamii yatawajibika kuchukua hatua za kuzuia matangazo yenye kurubuni na kupunguza hatari za kuwa mitandaoni.
Kati kesi za dharura ambazo zinahusiana na usalama wa taifa, mitandao mikubwa inatakiwa kufuata maagizo ya kuondoa maudhui ndani ya saa moja.
Kanuni kali zaidi zitatumika kwa mitandao yenye watumiaji zaidi ya milioni 10 kwa siku nchini Uturuki.
Ili kukabiliana na ukiukaji wa mara kwa mara, mitandao itahitajika kutumia akili mnemba ili kuhakikisha kwamba maudhui yaliyoondolewa awali hairudishwi.
Kanuni hizo zimeweka mfumo wa utekelezaji wa hatua kwa hatua.
Iwapo masharti hayatazingatiwa, matangazo mapya katika mtandao yatapigwa marufuku.
Iwapo ukiukaji utaendelea, mamlaka zinaweza kuitisha udhibitisho wa mahakama ili kupunguza kasi ya mitandao kwa asilimia 50 na mwishowe mpaka asilimia 90.
Mitandao ya michezo pia imejumuishwa, na kanuni zinazokataza michezo ambayo haina udhibiti wa umri.
Mitandao ya kigeni ya michezo yenye zaidi ya watumiaji 100,000 kwa siku, itatakiwa kuwakilishwa na mwanasheria nchini Uturuki.
Kanuni hizo zina lengo la kujenga mazingira salama, na yenye uwazi zaidi, huku kanuni hizo zikianza kufanya kazi miezi sita baada ya kutangazwa.






















