Iran imeshtumu vikali kile kinachosemekana kuwa uamuzi wa Israel kumteua balozi wake wa eneo la Somaliland, eneo lililojitenga ambalo Somalia linalitambua kama sehemu muhimu ya mipaka yake.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Esmaeil Baghaei ameeleza hatua hiyo kama “ukiukwaji wa wazi” wa sheria za kimataifa na kudharau mipaka na uhuru wa Somalia.
“Hatua kama hizi ni wazi zinakiuka makubaliano ya Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa,” Baghaei alisema Jumatatu, akionya kuwa hilo linaweza kuzidisha migawanyiko na ukosefu wa usalama katika kanda.
Baghaei alishtumu Israel kwa kuendeleza sera ambazo zina lengo la kuleta uchochezi ndani na nje ya Pembe ya Afrika.
Alisema hatua hii inaonesha mfumo mahsusi wa uingiliaji ambao unaweza kusababisha “ukosefu wa usalama katika mataifa ya Kiislamu na kuleta uchochezi baina ya nchi katika kanda.”
Hivi karibuni Israel ilimteua balozi wake wa kwanza Somaliland, ikiashiria kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia katika eneo hilo ambalo lilijitangazia uhuru kutoka kwa Somalia 1991 lakini bado halijatambuliwa na jamii ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa.
Serikali ya Somalia imekuwa ikikataa kutambuliwa kimataifa au kujihusisha na Somaliland kama taifa huru. Somalia imekuwa ikishtumu hatua hizo za ukiukwaji wa mipaka yake, ikisisitiza kuwa Somaliland bado ni sehemu ya Somalia.
Somaliland imekuwa na utawala wake wenyewe tangu kujitangazia uhuru 1991, ikiwa na serikali yake wenyewe, mifumo ya kisiasa, na taasisi za usalama.
Serikali ya Somalia mjini Mogadishu inaendelea kuitambua Somaliland kama sehemu muhimu ya Somalia na kuendelea kupinga uhusiano wowote na serikali za nje na eneo hilo, ikionya kuwa hatua kama hizo zinatatiza umoja wa Somalia na kukiuka sheria ya kimataifa.
Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Kiarabu na zile zenye idadi kubwa ya Waislamu pia zimeshtumu hatua hiyo ya Israel.
Katika taarifa ya pamoja iliotolewa siku ya Jumamosi, mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Qatar, Misri, Sudan, Libya, Bangladesh, Algeria, Palestina, Uturuki, Indonesia, Pakistan, Kuwait, Mauritania, Jordan, Oman, Lebanon, na Yemen waliielezea hatua hiyo kama “ukiukwaji wa wazi wa uhuru, umoja na mipaka ya Somalia.”
Jumuiya za kikanda, ikiwemo ile ya Ushirikiano wa mataifa ya Kiislamu na Umoja wa Afrika, pia zimetoa taarifa kushtumu hatua hiyo.


















