| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Polisi Afrika Kusini wawakamata watu zaidi 1,000 katika msako wa wahalifu
Msako huu wa sasa unakuja huku kukiwa na wasiwasi kuhusu viwango vya juu vya uhalifu nchini Afrika Kusini.
Polisi Afrika Kusini wawakamata watu zaidi 1,000 katika msako wa wahalifu
Vurugu za magenge na mitandao ya uhalifu zinaendelea kuwa tatizo kwa polisi Afrika Kusini. / Wengine
tokea masaa 3

Polisi katika mkoa wa Gauteng wa Afrika Kusini wamewakamata watu zaidi ya 1,000 katika msako wa mwishoni mwa wiki uliolenga maeneo yenye uhalifu zaidi, huku mamlaka zikiendeleza juhudi za kukabiliana na vurugu na utovu wa usalama.

Operesheni hiyo, iliyopewa jina la Shanela, iliwakamata watu 1,031 kwa makosa mbalimbali, ikiwemo yale yanayohusiana na dawa za kulevya, kuendesha ukiwa mlevu na ukiukaji wa sheria za uhamiaji.

Msemaji wa polisi wa mkoa Dimakatso Nevhuhulwi anasema watu 307 walikamatwa, ikiwemo 103 ambao hawakuwa na nyaraka sahihi za uhamiaji, washukiwa 54 wanahusishwa na dawa za kulevya, 72 kwa kuendesha gati wakiwa wamelewa na 32 kwa kuuza pombe haramu.

Katika hatua nyingine, maafisa waliwakamata washukiwa 724 kuhusiana na uhalifu wa vurugu, kuweka msisitizo kwa kile polisi walochokieleza kuwa harakati za kuondoa wahalifu sugu katika jamii.

Msako dhidi ya magenge ya wahalifu

Wale waliokamatwa wanatarajiwa kufikishwa katika mahakama mbalimbali katika siku zijazo.

Msako wa hivi sasa unakuja huku kukiwa na wasiwasi kuhusu viwango vya uhalifu katika baadhi ya maeneo nchini Afrika Kusini, ambapo magenge ya wahalifu na mitandao inaendelea kuwapa tabu polisi.

Mwezi uliopita, Rais Cyril Ramaphosa aliidhinisha vikosi 2,200 kutoka Jeshi la Afrika Kusini kusaidia polisi katika kukabiliana na magenge ya wahalifu, hasa jamii zilizoathirika zaidi na uhalifu.

Maafisa wanasema juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa kuweka usalama katika maeneo ambayo maafisa wa polisi pekee hawawezi kukabiliana na uhalifu.

CHANZO:TRT Afrika and agencies