Rais wa Kenya William Ruto ameidhinisha Mswada wa Marekebisho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, 2026 katika Ikulu ya Nairobi.
Sheria hiyo inaidhinisha kupunguzwa kwa VAT kama njia ya kuikomboa nchi kutokana na misukosuko ya kiuchumi inayosababishwa na mzozo wa Mashariki ya Kati.
"Tumepunguza VAT katika bei ya mafuta kutoka asilimia 16 hadi 8," Rais Ruto alisema.
"Tumechukua hatua hii ya dharura na muhimu kwa sababu kupanda kwa gharama ya mafuta kunaathiri vibaya bidhaa na huduma za watumiaji. Wakati punguzo hilo la VAT litakuwepo kwa muda wa siku 90, tumeweka kifungu kitakachotuwezesha kuongeza muda wa matumizi ya sheria ikiwa migogoro katika Mashariki ya Kati utaendelea kuathiri bei ya mafuta," aliongeza.
Kenya imeomba msaada wa haraka wa kifedha
Wakati huo huo Kenya imeomba msaada wa haraka wa kifedha kutoka kwa Benki ya Dunia ili kuisaidia kudhibiti misukosuko ya kiuchumi iliyosababishwa na vita vya Iran, Gavana wa wa Benki Kuu ya Kenya aliiambia Reuters.
Kama mataifa mengine ambayo yanategemea sana uagizaji wa nishati, nchi hiyo ya Afrika Mashariki inajitahidi kukabiliana na uhaba wa bidhaa muhimu ikiwa ni pamoja na petroli, huku ikidhibiti ongezeko la gharama ambalo linaweza kusababisha mfumuko wa bei.
Kenya ndiyo nchi ya kwanza kuthibitisha hadharani kwamba imewasilisha ombi rasmi kwa Benki ya Dunia, ingawa nchi kadhaa, kama vile Misri, zimesema zimewasiliana na wakopeshaji wa pande nyingi.
Mkuu wa IMF Kristalina Georgieva alisema kuwa zaidi ya nchi 12 zinatafuta usaidizi kutoka kwa Mfuko huo ili kukabiliana na mgogoro huo.
Ombi la fedha lilikuwa "muhimu," Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Kamau Thugge, aliiambia Reuters siku ya Alhamisi kando ya mikutano ya mataifa mbali mbali na Benki ya Dunia na IMF, bila kutoa maelezo ni pesa ngapi wanaomba.
"Msaada wowote ungekuwa pamoja na mkopo wa msaada wa kibajeti, ambao nchi na Benki ya Dunia zilikuwa zikijadili kabla ya kuzuka kwa mgogoro," alisema.
Usaidizi wa haraka ni neno linalotumiwa na Benki ya Dunia kwa mifumo yake ya kifedha inayotoa pesa kwa haraka na usaidizi wa sera ambao husaidia nchi kukabiliana haraka mishtuko au majanga.
Wiki iliyopita, Benki Kuu ya Kenya ilipunguza makadirio yake ya ukuaji wa 2026 hadi 5.3% kutoka makadirio ya awali ya 5.5%, ikisema kuwa vita vya Iran vilihatarisha sekta muhimu za uchumi mkubwa zaidi wa Afrika Mashariki.
















