| Swahili
UTURUKI
2 dk kusoma
Erdogan atuma salamu za rambirambi kufuatia shambulio la risasi shuleni katika jimbo la kusini
Mamlaka zimeanzisha uchunguzi kuhusu shambulio la silaha lililosababisha vifo vya watu 9 na wengine 13 kujeruhiwa.
Erdogan atuma salamu za rambirambi kufuatia shambulio la risasi shuleni katika jimbo la kusini
Rais Erdogan alisema: “Kwa masikitiko makubwa, katika shambulio hili la kusikitisha, tulipoteza watoto wetu mahiri na mwalimu aliyejitolea. / AA
tokea masaa 7

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan siku ya Jumatano alitoa salamu za rambirambi na kuwatakia afya njema kwa wale walioathiriwa na shambulizi la risasi shuleni katika mkoa wa Kahramanmaras nchini Uturuki, shambulio ambalo alisema "limehuzunisha sana Uturuki, haswa watoto wetu wapendwa."

Kupitia mtandao wa kijamii NSosyal, Erdogan aliandika: “Kwa masikitiko makubwa, katika shambulio hili la kusikitisha, tumepoteza watoto wetu mahiri na mwalimu aliyekuwa amejitolea kwa dhati. Namuomba Mwenyezi Mungu awarehemu waliopoteza maisha.”

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Mustafa Ciftci, shambulio hilo katika shule ya sekondari huko Kahramanmaras limesababisha vifo vya watu tisa na wengine 13 kujeruhiwa, sita kati yao wakiwa katika hali mahututi.

Rais pia alisema kuwa waendesha mashtaka wa umma, kwa kushirikiana na utawala wa kiraia pamoja na wakaguzi wa elimu, wanafanya uchunguzi kwa makini tangu tukio hilo lilipotokea, akiongeza kuwa suala hilo litafafanuliwa kikamilifu katika nyanja zote.

Gavana wa Kahramanmaras, Mukerrem Unluer, alisema kuwa shambulio hilo lilitekelezwa na mwanafunzi wa darasa la nane katika Shule ya Sekondari ya Ayser Calik, kwa sababu ambazo bado hazijajulikana.

Alieleza kuwa mwanafunzi huyo aliingiza silaha akiwa amezibeba kwenye begi na kuanza kufyatua risasi kiholela baada ya kuingia katika madarasa mawili. Aliongeza kuwa majeruhi wanaendelea kufanyiwa upasuaji na wengi wao wako katika hali mbaya. 

Mshukiwa huyo pia alifariki, ingawa haijabainika kama alijipiga risasi mwenyewe au aliuawa wakati wa vurugu.

Gavana huyo alisema kuwa silaha hizo huenda zilikuwa za baba wa mshukiwa, ambaye aliwahi kuwa askari. Inaripotiwa kuwa mwanafunzi huyo aliwasili shuleni akiwa na silaha tano.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Azerbaijan pia ilisema kupitia mtandao wa kijamii wa X kwamba wamesikitishwa sana na mashambulizi hayo ya shule katika “nchi ndugu ya Uturuki,” wakionyesha mshikamano na kutoa pole kwa familia za waathiriwa.

Rais wa Serbia, Aleksandar Vucic, pia alitoa taarifa kupitia akaunti yake ya mitandao ya kijamii akisema amehuzunishwa sana na tukio hilo, akitoa pole kwa Rais Erdogan na familia za waathiriwa, huku akiwatakia majeruhi kupona haraka.

CHANZO:AA