Zaidi ya vituo 80 vya nishati katika Mashariki ya Kati vimeharibiwa tangu kuanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran Februari 28, huku zaidi ya theluthi moja ya miundombinu yote ikitajwa kuwa imeathirika vibaya sana, amesema Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA).
Akizungumza katika hafla ya Baraza la Atlantiki huko Washington, DC, Fatih Birol alisema Jumatatu kwamba kiwango cha uharibifu katika maeneo ya mafuta, mitambo ya kusafisha, vituo na miundombinu ni kikubwa hivyo kurudi katika hali ya kawaida ya usambazaji itachukua muda hata kama mgogoro huo utamaliza sasa hivi.
"Hili ni mojawapo ya masuala muhimu zaidi, na tofauti na siku za nyuma, vifaa vingi vimeharibiwa vibaya," alisema, akiongeza kuwa IEA inafuatilia maeneo yote yaliyoathirika.
Birol, mwanauchumi wa Uturuki na mtaalamu wa nishati, alisema kurejesha usambazaji wa nishati ya kikanda mahali ilipokuwa kabla ya mgogoro inaweza kuchukua muda wa miaka miwili, akisisitiza kiwango cha uharibifu katika mfumo wa mafuta na gesi wa eneo hilo.
Alielezea msukosuko wa sasa kama "tishio kubwa zaidi la usalama wa nishati katika historia," akisema hasara katika usambazaji wa mafuta na gesi tayari inazidi ile iliyoonekana wakati wa uhaba wa mafuta duniani ya 1973 na 1979 na baada ya kuanza kwa vita vya Ukraine mnamo 2022.
Kutolewa kwa hifadhi ya mafuta ya dharura
Birol alisema dunia imepoteza takriban mapipa milioni 30 kwa siku ya usambazaji wa mafuta hadi sasa, ikilinganishwa na takriban mapipa milioni 5 kwa siku katika kila moja ya migogoro ya mafuta ya miaka ya 1970.
Katika gesi asilia, alisema usumbufu huo pia umezidi takribani mita za ujazo bilioni 75 zilizopotea tangu kuanza kwa vita vya Ukraine.
Kuhusu hatua za kukabiliana na dharura, Birol alisema IEA tayari imeratibu kutolewa kwa rekodi ya mapipa milioni 400 kutoka katika hifadhi ya kimkakati mwezi Machi, na kuiita hatua kubwa zaidi na ya haraka zaidi katika historia ya wakala.
Alisema anatumai kuwa hakutahitajika kutolewa kwa akiba nyingine ya dharura ya mafuta, lakini alisisitiza kuwa Shirika hilo liko tayari kuchukua hatua ikiwa hali ya soko itazidi kuwa mbaya.
Bado, alionya kuwa hifadhi za dharura pekee haziwezi kukabiliana na upotevu wa muda mrefu wa miundombinu, hasa katika nchi zilizo na uwezo mdogo wa kifedha au uwezo mdogo wa kuhifadhi.
Mbali na mafuta na gesi, alionya kuwa mzozo huo unatatiza usambazaji wa mbolea, kemikali za petroli, heliamu, na bidhaa nyengine muhimu katika usambazaji wa kimataifa.














