Waziri wa fedha wa Benin amepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa urais uliofanyika Aprili 12, akipata asilimia 94% ya kura zilizopigwa, kulingana na matokeo ya awali yaliyotolewa na tume ya uchaguzi siku ya Jumatatu.
Mkuu wa tume ya uchaguzi, Sacca Lafia, alisema kupitia televisheni ya taifa kulingana na asilimia zaidi ya 90% ya kura zilizohesabiwa, Romuald Wadagni anaongoza.
Kulingana na Lafia, wagombea Wadagni-Talata walipata kura 4,252,347, huku mgombea wa upinzani Paul Hounkpe akipata kura 269,433, ikiwa ni asilimia 5.95%.
Tume inasema matokeo hayo yalikusanywa kutoka vituo vya kupiga kura 15,814 kati ya vituo 17,463, ikiwa ni sawa na asilimia 90.55%.
Kimahesabu hakuna kitakachibadilika
Tume iliongeza kuwa “wigo ulioko kati ya wagombea ni mkubwa kiasi hakuna kitakachobadilika kimahesabu hata kama kura zilizobaki zitajumuishwa.”
Idadi ya waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 58.75%, huku watu 4,640,354 wakipiga kura kati ya 7,897,287 waliojisajili.
Kati ya hao, 4,522,756 zilikuwa kura halali, huku 117,598 zikisemekana kutopigwa kwa usahihi.
Tume imebaini kuwa upigaji kura ulifanyika kote nchini na katika vituo 14 vya nje ya nchi. Licha ya majaribio ya kutatiza mchakato huo katika baadhi ya maeneo kaskazini, inasema maafisa wa usalama walihakikisha kuwa wananchi wanapiga kura kwa uhuru.
Tume pia iliangazia matumizi ya majukwaa ya kidijitali, ambayo inasema ilihakikisha “upatikanaji wa haraka na usambazaji wa mahesabu.”
Mahakama ya katiba
Matokeo ya awali yatawasilishwa kwa Mahakama ya Katiba, ambayo ina mamlaka ya kuthibitisha na kutangaza matokeo ya mwisho.
Kulingana na utaratibu wa uchaguzi wa Benin, tume ina jukumu la kuandaa uchaguzi na kutangaza matokeo ya awali, huku Mahakama ya Katiba ikitatua mizozo ya uchaguzi na kuthibitisha matokeo ya mwisho.
Uchagui wa Aprili 12 ulifanyika kote nchini na nje ya nchi.

















