Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, na mwenzake wa Pakistan, Ishaq Dar, wamejadili kuhuzu mazungumzo yanayoendelea kati ya Marekani na Iran.
Fidan na Dar pia walijadili kupitia njia ya simu kuhusu hatua zitakazochukuliwa katika siku zijazo, kulingana na vyanzo vya kidiplomasia vya Uturuki siku ya Jumanne.
Zaidi ya watu 3,300 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel nchini Iran tangu Februari 28, kulingana na mamlaka za Iran.
Iran ilijibu kwa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yakilenga Israel, Iraq, Jordan, na kambi za kijeshi zilizoko katika nchi za Ghuba pamoja na baadhi ya miundombinu za nchi za Ghuba, kabla ya kusitishwa kwa mapigano kwa wiki mbili kutangazwa wiki iliyopita.
Marekani na Iran zilifanya mazungumzo ya moja kwa moja mjini Islamabad, Pakistan, siku ya Jumamosi yakilenga kumaliza mzozo wao, lakini mazungumzo hayo yalimalizika mapema Jumapili bila makubaliano yoyote.
Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, atatembelea Saudi Arabia na Uturuki kabla ya uwezekano wa kufanyika duru ya pili ya mazungumzo mjini Islamabad ili kumaliza vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel huku kukiwa na usitishaji dhaifu wa mapigano wa wiki mbili, ilisema taarifa rasmi siku ya Jumanne.
Pakistan, baada ya kufanikisha usitishaji wa mapigano wa wiki mbili wiki iliyopita, iliandaa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Marekani na Iran siku ya Jumamosi, ambayo yalimalizika bila makubaliano.
Vyanzo viwili vya serikali ya Pakistan vinavyofahamu juhudi za upatanishi viliiambia shirika la habari la Anadolu kuwa duru ya pili ya mazungumzo inatarajiwa kufanyika Islamabad “hivi karibuni” kwa mwaliko wa Pakistan.


















