Mwendesha mashtaka maalum wa Benin alisema Jumatatu kuwa anaandaa ombi la kutaka mwanaharakati wa uanamajumui maarufu Kemi Seba, kutaka arudishwe nyumbani baada ya kukamatwa na polisi mjini Pretoria, Afrika Kusini.
Seba, aliyezaliwa Ufaransa kwa wazazi wenye asili ya Benin, anatakiwa kwa madai ya kuchochea uasi baada ya kuunga mkono jaribio la mapinduzi lililotibuliwa mwezi Disemba.
Ataendelea kuwepo polisi hadi ombi lake la kutaka dhamana litakapokosikilizwa Aprili 29.
Mwanaharakati huyo mwenye umri wa miaka 45 alifikishwa mahakamani kwa muda mchache mjini Pretoria siku ya Jumatatu pamoja na mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka 18 na raia mmoja wa Afrika Kusini.
Kupitiliza muda wa kuishi
Chanzo kimoja karibu na Seba kiliiambia AFP kuwa mwanaharakati huyo ameishi Afrika Kusini kwa karibu miezi mitano na amepitiliza muda kwa miezi miwili.
Mwendesha mashtaka maalumu wa mahakama ya Benin wa kesi za uhalifu wa kiuchumi na ugaidi, Elonmario Metonou, alisema siku ya Jumatatu kuwa "sasa anaandaa" ombi la kupelekwa Benin.
‘Hakuna ombi la hifadhi ya kisiasa’
Mmoja wa wanasheria aliyemwakilisha Seba mahakamani Jumatatu, Sesedi Phooko, anasema wameshatuma maombi ya hifadhi ya kisiasa nchini Afrika Kusini. Hata hivyo, badaye ujumbe kwenye mtandao wa X wa Seba ulisema Phooko "hamuwakilishi Kemi Seba".
Juan Branco, mshauri wa Seba, ameiambia AFP kuwa majukumu ya wakili huyo yalikuwa yamemalizika kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.
"Kufikia sasa, hakuna ombi la hifadhi ya kisiasa ambalo limewasilishwa," alisema Branco.
Seba ana uraia wa Benin na Ufaransa lakini alipoteza uraia wale wa Ufaransa 2024. Ana hati ya kusafiria ya kidiplomasia iliyotolewa na utawala wa kijeshi wa Niger, ambao uliingia madarakani kupitia mapinduzi 2023.
Waendesha mashataka wameomba kesi hiyo kuahirishwa siku ya Jumatatu ili wapate kuchunguza uhalali wa pasipoti ya Seba, hadhi yake ya kuishi Afrika Kusini, na madai ya utakatishaji fedha.
Benin ilitowa hati ya kumkamata ya kimataifa kwa mwanaharakati huyo Disemba 12 baada ya kuunga mkono jaribio la mapinduzi lililotibuliwa ambapo wanajeshi waasi walidai kwenye televisheni kuwa wamempindua Rais Patrice Talon.
Baada ya jaribio la mapinduzi la Disemba 7, Seba alituma ujumbe wa video akisema ni "siku ya uhuru" kwa nchi yake.














