| Swahili
AFRIKA
1 dk kusoma
Tanzania: Fedha za sherehe za Muungano kutumika kukarabati miundombinu ya barabara
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifanyika tarehe 26 Aprili 1964, ukiziunganisha nchi hizi mbili huru kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tanzania: Fedha za sherehe za Muungano kutumika kukarabati miundombinu ya barabara
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba./Picha:@TZWaziriMkuu

Waziri Mkuu wa Tanzania Mwigulu Nchemba amesema kuwa, rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan ameelekeza fedha zilizokuwa zimepangwa kugharamia maadhimisho ya Sherehe za Muungano mwaka huu, zitumike kukarabati miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini humo.

Akizungumza Aprili 20, 2026, jijini Dodoma, Nchemba amebainisha kuwa maadhimisho ya Sherehe za Miaka 62 ya Muungano yatafanyika katika ngazi ya mikoa yote nchini ambapo viongozi wakuu wa kitaifa watafanya shughuli za kutembelea, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo.

Aidha, ameongeza kuwa wakuu wa mikoa wameelekezwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mipya, sambamba na kushiriki shughuli za usafi wa mazingira, upandaji miti na michezo mbalimbali.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifanyika tarehe 26 Aprili 1964, ukiziunganisha nchi hizi mbili huru kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano huu ulisainiwa na Rais wa kwanza wa Tanganyika, Julius Nyerere, na Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, ukilenga kuimarisha umoja wa Afrika na udugu wa nchi hizi mbili.

CHANZO:TRT Afrika Swahili