| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Mapigano yaripotiwa mashariki mwa DRC baada ya hatua kupigwa katika mazungumzo ya amani
Mamia ya raia wameondoka katika makazi yao kutokana na mapigano yaliyozuka mkoa wa Kivu Kaskazini huku Umoja wa Mataifa ukisema watu wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha.
Mapigano yaripotiwa mashariki mwa DRC baada ya hatua kupigwa katika mazungumzo ya amani
PICHA YA MAKTABA: Hali ya usalama mashariki mwa DRC bado ni tete. / Reuters

Mapigano mengine kati ya waasi wa M23 na vikosi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimesababisha mamia ya raia kuondoka katika makazi yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, vyanzo vya eneo hilo na Ofisi inayoshughulikia misaada ya Umoja wa Mataifa (OCHA) vilisema Jumanne.

Kulingana na vyanzo vya eneo hilo, vurugu hizo zilianza siku ya Jumapili na kuendelea hadi Jumanne katika eneo la Bukumbi, huko Masisi mkoa wa Kivu Kaskazini.

Mapigano hayo yanajiri huku hatua zikipigwa katika mazungumzo ya amani yanayoratibiwa na Qatar, nchini Uswisi, ambapo makundi hasimu yalikubaliana kuachia wafungwa waliowakamata katika kipindi cha siku 10 pamoja na kuhakikisha kufikishwa kwa misaada bila pingamizi.

Mazungumzo hayo yalihamishwa kutoka mjini Doha kutokana na vita vya Mashariki ya Kati.

“Vurugu zimesababisha mamia ya watu kukimbia makazi yao huku wengine wakijificha katika maeneo ya misitu ya karibu na wengine wakielekea katika maeneo ya jirani ya Walikale,” Ofisi ya Ofisi inayoshughulikia misaada ya Umoja wa Mataifa (OCHA) ilisema katika taarifa yake ya tathmini.

“Familia zilizoondoka katika makazi yao zinaishi katika mazingira mabaya sana, hasa kwenye maeneo ambayo kuna mapigano kwa sasa.”

Jeshi bado halijatoa taarifa yoyote kuhusu mapigano hayo ya sasa.

Mapema mwezi Aprili, wakazi wa vijiji kadhaa huko Ufamandu na Nyamaboko eneo la Masisi walikimbia makazi yao hadi eneo la Walikale kutokana na vurugu, kulingana na OCHA.

“Hii watu kuondoka katika makazi yao kila mara ni ishara ya ukosefu wa usalama ulioko Masisi na inaongeza matatizo kwa watu kupata mahitaji muhimu,” ilisema.

Waasi wa M23 wamekuwa wakiendeleza mapigano mashariki mwa DRC. Kundi hilo linadhibiti maeneo mengi mashariki mwa Congo, ikiwemo makao makuu ya mikoa ya Goma na Bukavu, ambayo yalidhibitiwa mapema 2025.

CHANZO:AA