| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
China imezipongeza nchi za Afrika zilizokataa kuruhusu ndege ya kiongozi wa Taiwan kutumia anga zao
Nchi kadhaa za Afrika zimefuta vibali vya safari za ndege, na kuathiri mpango wa safari iliyopangwa na kiongozi wa Taiwan kwenda Eswatini, mshirika pekee wa kidiplomasia wa Taiwan barani Afrika.
China imezipongeza nchi za Afrika zilizokataa kuruhusu ndege ya kiongozi wa Taiwan kutumia anga zao
Rais wa Taiwan, Lai Ching-te, alitarajiwa kufanya ziara nchini Eswatini kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 40 ya utawala wa Mfalme Mswati III./ / Reuters

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema Jumanne kuwa inatoa shukrani na pongezi kwa baadhi ya mataifa ya Afrika baada ya kufuta vibali vya ndege iliyokuwa imembeba kiongozi wa Taiwan.

China inaendelea kusisitiza kuwa Taiwan ni sehemu ya ardhi yake na inapinga juhudi zozote za kisiwa hicho kushiriki kama taifa huru katika majukwaa ya kimataifa.

Wizara hiyo imesisitiza kuwa uamuzi wao unaendana na kanuni ya “China moja” katika mahusiano ya kimataifa. China inaendelea kusisitiza kuwa Taiwan ni sehemu ya ardhi yake na inapinga juhudi zozote za kisiwa hicho kushiriki kama taifa huru katika majukwaa ya kimataifa.

Rais wa Taiwan, Lai Ching-te, alitarajiwa kufanya ziara nchini Eswatini kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 40 ya utawala wa Mfalme Mswati III pamoja na sherehe ya siku yake ya kuzaliwa ya 58. Hata hivyo, safari hiyo ilikatatizwa baada ya baadhi ya nchi za Afrika, zikiwemo Seychelles, Mauritius na Madagascar, kufuta vibali vya kuruhusu ndege yake kupita kwenye anga zao.

Kwa mujibu wa afisa wa Taiwan, uamuzi huo ulitokana na shinikizo kubwa la kiuchumi na kisiasa kutoka China, ambayo imekuwa ikiongeza juhudi za kuzuia ushirikiano wa kimataifa kati ya Taiwan na mataifa mengine.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema hatua hiyo inaonyesha uungwaji mkono wa mataifa hayo kwa kanuni ya “China moja” na kuongeza kuwa “hakuna anayeweza kuzuia mwelekeo wa kihistoria wa kuunganishwa kwa China.”

Eswatini, ambayo zamani ilijulikana kama Swaziland, ni miongoni mwa nchi 12 pekee duniani zinazotambua rasmi Taiwan kama taifa huru, baada ya China kushawishi mataifa mengi kukata uhusiano wa kidiplomasia na Taipei.

Kwa upande wake, serikali ya Eswatini ilisema inasikitishwa na kutokamilika kwa ziara ya Rais wa Taiwan, lakini ikasisitiza kuwa hatua hiyo haibadilishi uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

CHANZO:AFP