| Swahili
AFRIKA
1 dk kusoma
Zambia: Serikali yachukua mwili wa Edgar Lungu
Mvutano huo unaendelea huku pande zote zikishikilia misimamo yao kuhusu heshima na utaratibu wa mazishi ya kiongozi huyo wa zamani wa Zambia.
Zambia: Serikali yachukua mwili wa Edgar Lungu
Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu./Picha:Wengine

Serikali ya Zambia imesema kuwa imechukua mwili wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Edgar Lungu, huku mvutano kati yake na familia ya rais huyo wa zamani kuhusu mazishi yake, ukiendelea.

Kulingana na serikali ya Zambia, Lungu, ambaye alifariki dunia miezi 10 iliyopita nchini Afrika Kusini, anastahili kuzikwa kwa heshima za kitaifa kutokana na wadhifa wake wa zamani.

Serikali ya Zambia imesisitiza kuwa Lungu anastahili kuzikwa jijini Lusaka, katika eneo maalum, walipozikwa viongozi wengine wa kitaifa.

Hata hivyo, hoja hiyo imepingwa vikali na familia ya Lungu, ikisisitiza kuwa inataka mazishi ya faragha ya kifamilia.

Hapo awali, mahakama ya Afrika Kusini ilitoa ruhusa kwa serikali ya Zambia kurejesha mwili huo nchini Zambia kwa ajili ya mazishi ya kitaifa.

Mwanasheria Mkuu wa Zambia, Mulilo Kabesha, amesema kuwa mwili ulirejeshwa baada ya familia kushindwa kuendeleza rufaa yao.

Hata hivyo, msemaji wa familia, Makebi Zulu, amekanusha madai hayo, akisema kuwa rufaa ilikuwa bado inaendelea kwa mujibu wa sheria.

Mvutano huo unaendelea huku pande zote zikishikilia misimamo yao kuhusu heshima na utaratibu wa mazishi ya kiongozi huyo wa zamani.

CHANZO:TRT Afrika Swahili