Rais wa Nigeria Bola Tinubu amekubali kimsingi kuyafutia mashirika ya ndege ya ndani madeni yanayodaiwa na mawakala wa usafiri wa anga baada ya kufanyika kwa mazungumzo. Awali mashirika hayo yalitishia kusitisha huduma kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta, amesema siku ya Jumatano Waziri wa Huduma ya Usafiri wa Anga Festus Keyamo.
Mashirika ya usafiri wa ndege yametishia kusitisha huduma zote kuanzia Aprili 20 mpaka pale bei ya mafuta ya ndege itakapopungua, kwa mujibu wa Watoa Huduma wa Safari za Ndege nchini Nigeria (AON).
Rais Tinubu ametaka kuwasilishwa kwa ombi rasmi haraka iwezekanavyo, na asilimia ya punguzo la deni itakayopangwa na yeye mwenyewe, amesema Keyamo.
Serikali pia itaunda kamati ya kupitia upya kodi, ushuru, na ada zinazotozwa katika tiketi za ndege, ili kupendekeza punguzo litakalopunguza ugumu wa uendeshaji kwa mashirika na abiria.
Wauzaji mafuta wanatakiwa kukaa na maafisa wa serikali Alhamisi ili kujaribu kutatua mgogoro huo wa bei ya mafuta haraka iwezekanavyo, amesema katibu wa Wizara ya Nishati Patience Oyekunle baada ya mazungumzo ya Jumatano.
Kupanda kwa bei ya mafuta duniani kumetokana na athari za vita vya Iran, hivyo mashirika ya ndege kulazimika kupandisha nauli.














