| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Shirika la Uingereza latoa onyo kufuatia ‘kutekwa' kwa meli karibu na pwani ya Somalia
Kituo cha Pamoja cha Taarifa za Baharini (JMIC) kimepandisha kiwango cha tishio kuwa "kikubwa" katika Pwani ya Somalia.
Shirika la Uingereza latoa onyo kufuatia ‘kutekwa' kwa meli karibu na pwani ya Somalia
Meli ya mizigo inaripotiwa kutekwa nyara karibu na pwani ya Somalia./ / AP

Meli ya mizigo imeripotiwa kutekwa karibu na pwani ya Somalia, baada ya watu wanaoripotiwa kuwa maharamia kuchukua udhibiti wa meli na kuilekeza ndani ya maji ya eneo hilo mwishoni mwa, hii ni kwa mujibu wa Shirika la Uingereza linaloshughulikia masuala ya bahari (UKMTO).

Tukio hilo liliripotiwa takriban maili za baharini sita (sawa na kilo mita 11.1) kaskazini-mashariki mwa Garacad, Somalia, UKMTO iliandika katika mtandao wa kijamii wa X.

“Imeripotiwa kuwa watu wasioidhinishwa wamechukua udhibiti wa meli ya mizigo na kuielekeza ndani ya maji ya mipaka ya nchi,” ilisema taarifa hiyo.

UKMTO imezishauri meli zilizo katika eneo hilo kuwa waangalifu kutokana na kuongezeka kwa hatari za kiusalama.

‘Piteni kwa tahadhari’

“Kwa sababu ya kuongezeka kwa tishio la uwezekano wa shughuli za Vikundi vya Uharamia (PAG), meli zinashauriwa kupita kwa tahadhari na kuripoti mienendo yoyote inayotia shaka,” ilisema.

Mamlaka zinaendelea kuchunguza tukio hilo.

Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu wafanyakazi wa meli, mzigo wake, wala utambulisho wa waliohusika katika utekaji huo.

Wakati huohuo, JMIC imepandisha kiwango cha tishio kuwa “kikubwa” katika Pwani ya Somalia,” ikionyesha kuwa uwezekano wa shambulio sasa ni mkubwa.

“Meli ya bidhaa za mafuta inaripotiwa kushikiliwa na maharamia katika pwani ya kaskazini-mashariki mwa Somalia. Hakuna majeruhi yaliyoripotiwa. Aidha, Kikundi cha Uharamia kinaripotiwa kuwa kinafanya shughuli katika eneo la Somalia. Meli zilizo karibu zinashauriwa kuongeza uangalizi na kupitia mwongozo wa BMP-MS,” JMIC ilisema katika taarifa yake ya Aprili 26.

Mwelekeo mpya wa usalama wa baharini

Wachambuzi wanasema onyo hilo linaashiria mwelekeo unaotia wasiwasi katika eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likihusishwa na changamoto za usalama wa baharini.

Katika kipindi cha shughuli za uharamia nchini Somalia kati ya mwaka 2008 na 2011, zaidi ya mashambulizi 200 yalirekodiwa, huku makundi yenye silaha yakishambulia meli, kuwateka wafanyakazi wake na kudai fidia.

Tishio hili jipya linaibuka wakati njia muhimu za kimataifa za usafirishaji tayari ziko chini ya shinikizo, hasa katika Mlango-Bahari wa Hormuz, ambako mvutano unaohusisha Marekani, Israel na Iran umeathiri pakubwa usafiri wa baharini.

CHANZO:TRT Afrika and agencies