Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaadhimisha miaka 10 tangu kifo cha Papa Wemba, mmoja wa wasanii wakubwa wa muziki barani Afrika.
Jina lake halisi, Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba, alijulikana kama "Mfalme wa Rumba Rock" na muanzilishi wa muziki wa kisasa wa Congo.
Alianza katika bendi ya magwiji ya Zaiko Langa Langa mwishoni mwa miaka ya 1960 kabla ya kuanzisha kundi lake la Viva La Musica, na hapo ndipo umaarufu wake wa kimataifa ulipoanzia.
Papa Wemba hakuimba tu, alijenga utamaduni.
Aliongoza harakati za Mitindo, La Sape. Mtindo wa maisha wa ulimbwende, mitindo ya wabunifu, na kujiamini.
Muziki wake ulichanganya Rumba, ushawishi wa Soukous Pop Na vibao vyake vilimfanya kuwa nyota wa kimataifa wa Afrika, akizunguka Afrika nzima na nje ya bara.
Na kama alivyoishi, jukwaani akifanya kile alichopenda, pia alikufa jukwaani akifanya hivyo.
Mnamo Aprili 24, 2016, wakati wa onesho la moja kwa moja katika ukumbi wa FEMUA mjini Abidjan Papa Wemba alianguka na kupoteza fahamu akiwa jukwaani.
Baadaye alitangazwa kuwa amefariki - akiwa na umri wa miaka 66. Tangazo lililoishitua Afrika ...
Bingwa ameondoka
Wiki hii kote DRC na kwengineko, mashabiki wanaadhimisha kumbukumbu ya miaka 10 kwa njia ya matamasha ya heshima na filamu juu ya maisha yake na mikusanyiko ya ukumbusho.
Rais FelixTshisekedi alikuwa sehemu ya waliohudhuria sherehe katika kijiji cha Molokai huko Matonge Kinshasa inayoaminiwa kuwa asasi ya kihistoria ya bendi ya Papa Wemba Viva la Musica kama sehemu ya ukumbusho wa muongo mmoja tangu kuondoka kwa gwiji huyo.
Wasanii kote barani Afrika pia wanasherehekea mchango wake kwenye Afrobeat ya kisasa, rumba ya Congo na utamaduni wa utumbuizaji katika jukwaa la Kiafrika.
Papa Wemba alisaidia kufafanua utambulisho wa muziki wa Kiafrika kwenye jukwaa na mtindo wa kimataifa kama sehemu ya utamaduni wa muziki, na miaka 10 baadaye sio kumbukumbu tu bali bado anashawishi muziki wa Kiafrika leo.













