Milipuko miwili ilisikika na milio ya risasi kuendelea karibu na kambi kuu ya kijeshi ya Mali, Kati, nje ya mji mkuu Bamako, na wanajeshi kuweka vizuizi barabarani, walioshuhudia wanasema.
Milio ya risasi ilisikika maeneo mbalimbali ya taifa hilo la Afrika Magharibi siku ya Jumamosi, ikiwemo eneo la Kati, sehemu ambapo kuna makazi ya kiongozi wa kijeshi Jenerali Assimi Goita, walioshuhudia na chanzo cha kijeshi kiliiambia AFP.
Haikufahamika mara moja chanzo cha milipuko hiyo, na hakuna kundi lililokiri kuhusika na shambulizi hilo.
Nchi hiyo ya kati ya Sahel inapambana na mashambulizi ya kundi la Afrika Magharibi lenye uhusiano na makundi ya kigaidi ya Al Qaeda na Daesh. Pia inakabiliwa na tatizo la muda mrefu la kihistoria la watu wa jamii ya Tuareg wanaotaka kujitenga kaskazini mwa nchi.
Serikali ikiongozwa na Assimi Goita imeegemea upande wa mamluki wa Urusi kwa usaidizi wa masuala ya usalama huku awali wakiimarisha ushirikiano wa ulinzi na mataifa ya Magharibi. Hivi karibuni, imeanza ushirikiano na Marekani.
Reuters inaripoti kuwa mwezi Machi Mali na Marekani walikuwa karibu kufikia makubaliano ambayo yangeruhusu Marekani kuanza kupeleka ndege na droni katika anga ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwa ajili ya kupata taarifa za kijasusi kuhusu makundi yenye silaha na yale ya kigaidi.















