Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amekutana na mkuu wa majeshi wa Pakistan Asim Munir mjini Islamabad siku ya Jumamosi, huku juhudi zikiendelea za kufufua mazungumzo ya amani yaliyokwama kati ya Marekani na Iran kwa lengo la kumaliza vita vyao vya wiki nane.
Mkutano huo, kulingana na video fupi iliotolewa na ubalozi wa Iran kwa mtandao wa kijamii wa Marekani wa X, pia ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan Mohsin Naqvi, Mshauri wa Masuala ya Usalama na Mkuu wa Ujasusi Luteni Jenerali Asim Malik, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran Esmaeil Baghaei, na balozi wa Iran Reza Amiri Moghadam.
Pamoja na ubalozi kutotoa taarifa zaidi, vyanzo vya Pakistan viliiambia Anadolu kwua pande zote mbili zilijadili masuala ya kurudi katika duru ya pili ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran katika siku za hivi karibuni.
Araghchi aliwasili Pakistan Ijumaa jioni kwa kile ambacho maafisa wa Pakistan wanasema ni kutoa nafasi kwa duru ya pili ya majadiliano. Duru ya kwanza ilifanyika mjini Islamabad wiki mbili zilizopita, lakini hakuna makubaliano yaliyofikiwa. Mazungumzo hayo yalianza baada ya Pakistan kuwezesha upatikanaji wa usitishaji mapigano kwa wiki mbili Aprili 8, ambapo baadaye muda uliongezwa na Rais wa Marekani Donald Trump.
Araghchi pia atafanya mazungumzo na Waziri Mkuu Shehbaz Sharif na Waziri wa Mambo ya Nje Ishaq Dar.
Wakati huohuo, Ikulu ya Marekani imesema mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff na mshauri Jared Kushner pia watasafiri kuelekea Pakistan siku ya Jumamosi.
Iran imekataa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani, na kusema kuwa kero zao zitawasilishwa kwa Pakistan.













