Rais wa Uganda Yoweri Museveni amehimiza kila mtu kuwa nyumbani kuanzia saa moja usiku tarehe tisa mwezi Mei ili apate kuhesabiwa / Picha kutoka Ikulu ya Uganda

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametangaza kuwa nchi yake itafanya sensa ya kitaifa ya watu na makazi mwaka 2024.

"Sensa ya Watu na Makazi imepangwa kufanyika usiku wa Mei tarehe 9 na 10 mwezi Mei mwaka 2024. Nadhani kuhesabu watu kutaanza saa sita usiku kwa sababu saa moja jioni baadhi ya watu watakuwa bado kwenye starehe, " rais Museveni amesema akizindua hafla hiyo jijini Kampala nchini Uganda.

Serikali inasema siku hiyo itaadhimishwa kama siku ya mapumziko ili kuwezesha idadi kubwa ya wananchi kuhesabiwa.

Zaidi ya watu 120,000 watapewa kazi ya kuhesabu watu ikiwa serikali inalenga zaidi vijana.

"Huwezi kuwapangia watu usiowajua, Sensa inasaidia kwa takwimu katika hili. Pia inaangazia uwezekano wa uwekezaji kwani wawekezaji watakuwa na sifa za idadi ya watu. Sensa inatusaidia kujua watu wako wapi, mali zao na wanachofanya,"

Ofisi ya takwimu ya Uganda, (Uganda Bureau of statistics), UBOS inasema kuwa sensa inaleta maelewano kati ya serikali za mitaa na serikali kuu, sekta binafsi, viongozi wa dini na wengine.

"Inakadiriwa kuwa, idadi ya watu nchini Uganda inafikia milioni 42.6, ongezeko kutoka milioni 34.6 lililorekodiwa wakati wa sensa ya 2014," Dkt. Chris Mukiza mkurugenzi mkuu wa UBOS amesema.

"Hata hivyo, sensa ijayo ya Mei 2024 itatoa taswira sahihi na ya kina zaidi ya mahali tupo kama nchi," ameongezea, "Itakuwa ni sensa ya kwanza ya kidijitali na matokeo yatatolewa kwa muda wa takriban miezi sita."

Serikali tayari imejitolea kufadhili zaidi ya dola milioni 85 kufanikisha mpango huu. Hii ni asilimia 98 ya fedha zinazohitajika. Salio la zaidi ya dola milioni 3.4 linatarajiwa kuongezwa kwa muda.

Kwa mara ya kwanza hesabu ya idadi ya watu itafanywa kwa njia ya kidijitali.

UBOS imesema matokeo ya sensa ya kiteknolojia yatatoka mwezi Juni 2024, matokeo ya muda kuwasilishwa Septemba 2024 na matokeo ya mwisho Desemba 2024.

Sensa ya 2024 itakuwa zoezi la sita kufanyika tangu Uganda kupata uhuru mwaka 1962.

Sensa ya mwisho ilikuwa mwaka 2014.

TRT Afrika