Rais wa Uganda Yoweri Museveni amemuandikia barua mwenzake wa Marekani Joe Biden ikiwa ni majibu kwa Biden kuamua kuondoa Uganda katika mpango wa pamoja wa biashara, AGOA.
Rais alithibitisha hilo alipokutana na William Popp, Balozi wa Marekani nchini Uganda katika Ikulu ya Uganda mjini Entebbe.
Marekani ilitangaza kuiondoa Uganda kwenye utaratibu wa kunufaika na AGOA kuanzia Januari 2024, baada ya nchi hiyo kupitisha sheria dhidi ya mapenzi ya jinsia moja Mei mwaka huu.
Vikwazo vyengine vya viza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken ametangaza kuwa Marekani itaongeza vikwazo vya viza kwa maofisa wa serikali wa Uganda, wa sasa na waliokuwa serikalini,
"Vizuizi vya viza itajumuisha maafisa wa sasa au wa zamani wa Uganda au wengine ambao wanaaminika kuwajibika, au kushiriki katika, kudhoofisha mchakato wa kidemokrasia nchini Uganda au kwa sera au vitendo vinavyolenga kukandamiza watu waliotengwa au walio hatarini," taarifa ya Blinken ilisema.
Marekani inasema watu wa karibu na familia ya maafisa wanaolengwa huenda pia kuwekwa chini ya vizuizi hivi.
Baada ya uchaguzi wa urais wa Uganda wa 2021 ambayo Marekani ilisema haukuwa wa haki, Blinken alitangaza sera ya kuzuia viza inayolenga wale wanaoaminika kuwajibika, au kushiriki katika kuhujumu mchakato wa demokrasia nchini Uganda.