Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Kundi la The Jacksons 5 limepoteza mwanafamilia mwingine, Tito Jackson.
Hilo ni pigo jengine kwa familia hiyo ya wanamuziki waliokuwa na vipaji vikubwa ulimwenguni, ikiwa ni miaka 15 baada ya kifo cha Michael Jackson.
Tito, ambaye jina lake halisi ni Toriano Adaryll Jackson alizaliwa Oktoba 15, 1953 huko Gary Indiana, nchini Marekani na alikuwa ni mtoto wa tatu kuzaliwa kati ya 9 wa mzee Joe Jackson na Katherine Esther Jackson.
Alikuwa ni mmoja wa waanzilishi wa kikundi hicho kilichoasisiwa mwaka 1964 na Mzee Joe Jackson mwenyewe.
Kama ilivyo kwa ndugu zake wengine; Jackie, Jermaine, Marlon na Michael, Tito alikuwa na mchango mkubwa kwenye kundi la The Jacksons 5, akijulikana sana kwa kupiga gitaa na uimbaji wa sauti nzuri.
Licha ya kuungana na ndugu zake wa kiume katika The Jacksons 5, Tito alikuwa na dada zake ambao pia ni wanamuziki, yaani Janet Damita Jo Jackson na La Toya Yvonne Jackson.
Alishirikiana na ndugu zake kutoa vibao vikali vilivyotesa enzi hizo vikiwemo ABC, The Love You Save, I'll Be There na Never Can Say Goodbye wakati ndugu hao watano wakiwa chini ya lebo ya Motown.
Enzi za uhai wake, Tito Jackson alijaaliwa kupata watoto watatu ambao ni Taj, Taryll na TJ ambao waliunda kundi maarufu la 3T.
Kundi hilo lilijizolea umaarufu kupitia nyimbo zao mbalimbali zikiwemo, Anything wa mwaka 1995 na I Need You wa mwaka, ambao walimshirikisha baba yao mdogo Michael Jackson.
Katika mahojiano yake na The Associated Press, yaliyofanyika Disemba 2009, Tito Jackson alinukuliwa akisema kuwa kifo cha mdogo wake, Michael Jackson kilichotokea June 25, 2009, kiliileta familia ya The Jacksons karibu zaidi.
Tito alifariki dunia Septemba 15, 2024 kwa mshtuko wa moyo wakati akiendesha gari kutoka eneo la New Mexico kuelekea Oklahoma nchini Marekani.