Lucas Mkenda almaarufu Mr Nice./Picha: Wengine

Na Paula Odek

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Kuku kapanda Baiskeli, Bata kavaa Laizoni…..Fagilia, Fagilia Bongo, Wa waaaa!

Leo nataka nikurudishe nyuma kidogo kwa kumbukumbu mujarab, ya nguli aliyetikisa Bongo Fleva kwenye miaka ya 2000.

Huyu si mwingine, bali ni Lucas Mkenda, almaarufu Mr Nice, ambaye kwa hakika, alitupagawisha vilivyo miaka hiyo, hasa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.

Akiwa amezaliwa wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, nchini Tanzania, miaka 46 iliyopita, alijipatia elimu yake ya msingi katika shule ya Ilala Boma jijini Dar es Salaam, na kisha kurejea mkoani Kilimanjaro kwa elimu ya Sekondari.

Mr Nice ndiye muasisi wa mtindo wa TAKEU./Picha: Wengine

Mr Nice ndiye muasisi wa mtindo maarufu wa TAKEU, wenye kumaanisha Tanzania, Kenya na Uganda ambao, ama kwa hakika ulikonga nyoyo za mashabiki wengi wa Bongo Fleva miaka hiyo.

Wimbo wa Friday Night, ndio ulimtambulisha rasmi Mr Nice kwenye tasnia ya Bongo Fleva na nyingine nyingi kama vile Kidalipo, King’asti, Kikulacho na ule wa Fagilia ambao uliwahi pia kutumiwa na Brass Band nchini Kenya.

Tangu alipoibukia kwenye tasnia ya muziki, nyimbo za Mr Nice zilichezwa na watu wa marika yote, hasa kutokana na kutumia michezo ya wakati uleeeee, kama vile ‘kidalipo’ na ‘Kuku kapanda Baiskeli’.

Inaaminika kuwa Mr Nice ndiye msanii aliyekuwa na mafanikio makubwa ya kifedha kwa wakati huo./Picha: Wengine

Hutokuwa kuwa umekosea ukisema kuwa Mr Nice, alikuwa ndiye Diamond Platinumz wa kipindi hicho, kwani alikuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki jukwaa.

Hakika msanii huyu alikamata enzi hizo, na inasemekana ndiye msanii aliyekuwa na mafanikio makubwa ya kifedha kwa wakati huo.

Wengi mtakumbuka uhasama kati ya Mr Nice na Dudubaya, ambapo mara kwa mara, Dudubaya alikuwa akivamia jukwaa la Mr Nice na kumshambulia msanii huyo.

Hata hivyo, wawili hao waliweka tofauti zao pembeni, kwani mwaka 2014 walianza kufanya ziara za kimuziki pamoja.

Kwa kinywa chake mwenyewe, Mr Nice anasema kuwa aliwahi kupewa sumu ili afe, kutokana na sababu asiyoijua hadi hii leo.

Mr Nice, ambaye amezaliwa wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, nchini Tanzania, miaka 46 iliyopita, alijipatia elimu yake ya msingi katika shule ya Ilala Boma jijini Dar es Salaam, na kisha kurejea mkoani Kilimanjaro kwa elimu ya Sekondari./Picha: Wengine

Kwa sasa, Mr Nice amehamishia makazi yake nchini Kenya, akiwa amehamia huko kutoka mwaka 2020, akitokea nchini Uganda.

Pia, inasemekana kuwa nguli huyo wa Bongo Fleva, amefungua studio yake mwenyewe katika Kaunti ya Machakos.

Mr Nice anasema kuwa anajisika nyumbani zaidi awapo nchini Kenya kuliko akiwa nchini Tanzania, na kwamba Watanzania hawamkubali tena kama ilivyo kwa Wakenya.

Zipo tetesi pia, kuwa Mr Nice amepata ‘mwandani wa Kikenya’.

Mbali na muziki, Mr Nice ni hodari sana katika sanaa ya uchoraji.

Amewahi kunukuliwa akisema kuwa anachora vizuri zaidi kuliko uimbaji.

TRT Afrika