George Ekombe anamwambia mteja wake wa mwisho aharakishe kwa sababu anahitaji kufunga duka lake na kwenda mazoezini.
Mwanaume huyu mwenye umri wa miaka 24 ana duka ndogo la chumba kimoja ambapo watu hulipa kwa ajili ya kucheza michezo kwenye televisheni ndogo aliyopachika ukutani.
Kwa siku nzuri anapata dola 2, chini kabisa ya kile alichokuwa akivuna alipokuwa mitaani kama mwizi.
"Haya ndiyo maisha yangu sasa," George anaiambia TRT Afrika, "Ni vigumu sana kwa sababu wakati mwingine sipati hata hizo dola mbili, lakini nitaendelea na hili kwa sababu nimeapa sirudii tena uhalifu."
George alitoroka nyumbani akiwa na umri wa miaka 7 ili kujitunza kwa sababu anasema alihisi "amekuwa mwanaume".
"Baada ya kuwa mtaani kwa miaka miwili nilijifunza ujuzi wa kuiba hasa simu kutoka kwa mifuko ya watu. Kuna watu mijini ambao walikuwa wananunua hizo simu za wizi. Nikiwa mdogo kupata kati ya dola 30 na 100 kwa siku moja ilikuwa kama nimefika mbinguni," aeleza George.
Pesa zote zilizopatikana kwa siku moja zilipotea kwenye pombe na starehe zingine.
"Siku moja , nakumbuka vizuri sana,ilikuwa Alhamisi, mmoja na marafiki zangu wawili walituambia kwamba wamepanga uhalifu mkubwa ambao utatuondoa kwenye umaskini milele, tulifikiri ni kuiba televisheni au redio,"- kama anaelezea anapotea katika maelezo bila kuzingatia muda, kabla ya kuanza tena , “tulimshambulia mwanaume ambaye mwenzetu alisema alikuwa muajiri wake na alikuwa ana roho mbaya.”
George anasema alianza kuwa na mawazo ya pili kuhusu maisha ya mtaani walipogundua kuwa mwenzake alikuwa ameleta bunduki kwa operesheni hii.
"Silaha haikuwa mtindo wetu, sisi tulizoea tu kunyakua simu na kuwapora watu, lakini hatukuwahi kujiingiza katika matumizi ya silaha. Niliogopa sana kwa sababu bunduki si jambo zuri, mitaani tunaamini bunduki itakupeleka kwenye kifo chako mwenyewe.”
Mnamo 2017 wenzake wawili wa mtaani walipigwa risasi na polisi walipokuwa wakiiba mchana kweupe. George alijua safari yake pia ndiyo ingekuwa haibadilika.
“Nilihamia kijiji hiki cha Kibarage, kuishi bila kazi katika makazi yasiyo rasmi hivyo ilifanya kwangu kuwa vigumu kuacha kufikiria uhalifu, lakini kocha wetu Aaron alinifuata na kuniomba nijiunge na timu yake ya soka. Aaron amekuwa kama baba ambaye sikuwahi kuwa naye. Ni yeye alinisaidia kufungua hii biashara yangu."
Nilijituma Jela
George anapofunga duka lake, anamwita Setrick Isichi, mchezaji mwenzake wa timu ambaye anafanya kazi katika duka jirani.
Setrick mwenye umri wa miaka 26 ameketi katika duka linalomilikiwa na rafiki yake akisubiri fursa yoyote ya kupata pesa. Duka hilo huuza maji kwa wakazi wa eneo hilo. Yeye husaidia watu kubeba maji hadi nyumbani kwao na siku nzuri anaweza kupata hela kidogo kutokana na zoezi hilo.
"Niliingia katika ulimwengu wa uhalifu nikiwa na miaka 15, nilikuwa kijana wa mitaani, nilitamani sana pesa ambazo wenzangu mitaani walikuwa wanapata walipoiba," Setrick anaelezea TRT Afrika.
Jaribio lake la kwanza lilikuwa kumpokonya simu mtu aliyekuwa kwenye gari lililokuwa likisogea. Mafanikio ya kasi hiyo yalimuwekea msingi wa wizi.
Misuli ya uso wake inakaza na anainama mbele kabla ya kuendelea kwa sauti ya chini,
"Siku moja mwaka wa 2012, rafiki yangu mmoja alimpokonya mtu simu na kutoroka vizuri na hakushikwa, kwa hiyo mimi pia nilijaribu kufanya hivyo," anaeleza huku machozi yakimlenga.
"Lakini nilipokuwa nikijaribu kukimbia, nilikamatwa na wanaume wawili, ambao walianza kupiga kelele kwamba mimi ni mwizi na katika sekunde chache tu kundi la watu lilikusanyika na kuanza kunishambulia,” Setrick anasema.
Athari za mashambulizi ya halaiki yanaonekana wazi kwa alama nyingi usoni mwake na makovu mengine kichwani.
Polisi walimuokoa Setrick kutoka kwa kundi la watu, wakampeleka hospitali na baadaye akapelekwa gerezani.
Miaka miwili ya maisha gerezani ilikuwa ngumu, na hakuwa na mtu wa kumtembelea, lakini iliweka msingi wa mageuzi yake. Alirudi shuleni akiwa huko. Anatabasamu huku akieleza jinsi mkuu wa gereza alivyompa sungura 3 kuwafuga na wakati anaachiliwa walikuwa wameongezeka hadi 50.
Baada ya kuachiliwa, Setrick alirejea nyumbani katika kijiji cha Kibagare, akidhamiria kujiepusha na uhalifu. Alioa na kupata mapacha. Alitegemea kazi za mijengo na hata akajiunga na timu ya kandanda ya kijiji hicho.
Hata hivyo, watoto wake wote wawili walikufa siku moja, kabla hata ya kufika umri wa mwaka mmoja.
"Ninajuta kuwaibia watu na wengine kuwaumiza,watoto wangu walipofariki, nilifikiri dunia inalipiza kisasi kwa sababu ya maovu niliyowafanyia watu," anasema huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.
Mnamo Novemba 2022, polisi wa Kenya walipiga marufuku wachuuzi na familia za mitaani kumiliki na kufanya biashara kwenye madaraja ya miguu ndani ya mji mkuu, Nairobi.
Wakazi pia walitahadharishwa kuhusu maeneo ndani ya jiji ambayo yanayokumbwa na matukio ya ujambazi.
Wengi wa wahalifu wa zamani ambao TRT Afrika ilizungumza nao katika kijiji cha Kibagare walisema kuishi katika makazi yasiyo rasmi kama yao kunaweza kumvuta kwa urahisi kijana kwenye uhalifu.
Umaskini uliokithiri, kuacha shule, shinikizo la rika, ukosefu wa ajira, uvivu na hamu ya kuwa na maisha rahisi ,vijana hao walisema ni baadhi ya sababu zinazowafanya watoto wengi wachanga kutumbukia katika uhalifu tangu wakiwa wadogo.
Nguvu ya Soka
Uwanja wa mpira wa kijiji cha Kibagare uliojaa vumbi , huwa na shughuli nyingi kuanzia saa kumi jioni kila siku. Wakazi kutoka makaazi yasiyo rasmi hapa huja kufanya mazoezi, wengine kwa vikundi huku wengine mmoja mmoja.
Watoto pia hujiunga kwenye michezo na mipira yao pia.
Kwa baadhi ya wakazi ni mahali pa kukutana na kuzungumza wanapotazama shughuli za wengine uwanjani.
Aaron Kifogo anapuliza kipenga kwa utaani kutangaza kuwasili kwake. Aliunda ‘Kibagare Sportiff’, timu ambayo George na Setrick wamo.
Wachezaji wake wanamwita “FIESCO”, jina la utaani alilojiundia yeye mwenyewe.
Wengine wanamkumbatia, wengine kumpiga mabegani huku wakijipanga kusikiliza maelekezo yake ya siku.
“Ninasukumwa na mapenzi na uchungu,” Aaron aelezea TRT Afrika, “nikiwa nimezaliwa na kulelewa katika makazi haya yasiyo rasmi, nimeona athari ya uhalifu kwa vijana. Marafiki wangu wengi wamepigwa risasi au kufa kutokana na uhalifu. Nilikamatwa kwa ulaghai pia nilipokuwa mdogo. Baada ya kuachiliwa niligundua kwamba nilipaswa kubadilika kwa sababu dada na kaka yangu wananitegemea.”
Mnamo 2018 Aaron, ambaye sasa ameoa na ana mtoto mmoja, alianzisha mradi unaoitwa "Kampeni ya Vijana dhidi ya Uhalifu," ili kufikia vijana wengi kama yeye ambao waliamini uhalifu ndio chanzo pekee cha mapato.
Anasema changamoto kubwa ni kwamba hakuwa na majibu wakati vijana walipomuuliza angewapa nini badala ya uhalifu.
“Ningemwona kijana ambaye bado ni mhalifu na kumtia moyo ajiunge nasi. Ningewatia moyo kwamba kandanda itatusaidia kujiepusha na dawa za kulevya, jela na kifo kutokana na uhalifu. Kuna faraja tukikutana kwa timu yetu kwa sababu hakuna atakayekuhukumu hapa, asili mia tisini yetu tumekuwa wahalifu."
Timu ilianza na vijana 15 na baada ya muda imeongezeka kuwa na 40.
George anafanya mazoezi na timu lakini wakati wa mashindano anakuwa mtangazaji wao “Michezo imeniokoa kutoka kwa risasi na jela. Mpira huondoa mawazo ya ujambazi, ubakaji na tamaa mbaya ya kile usichoweza kumudu." George anaielezea TRT Afrika.
Kwa wengine, kama Isichi, mchezo huu umemfanya ajisikie anathaminiwa.
“Michezo imeniunganisha na marafiki wengi. Imeniwezesha kuzunguka nchi nzima kwa ajili ya mashindano. Kuna sehemu nimeenda, na watu wasionifahamu walinishangilia na kunipongeza kwa kucheza vizuri. Kufurahiwa ni jambo ambalo sikuwahi kupata nilipokuwa mhalifu,” asema huku akitabasamu sana.
Wanachama wake humuita ‘Kocha wa simu’, kwa sababu huwa anapiga simu kila mara kuazima sare na viatu vya timu nyingine kila wanapokuwa na mashindano.
Takriban miaka minne iliyopita wakati timu ya soka ya 'Kibagare Sportiff' ilipoanza kijiji kilikuwa kinapoteza angalau vijana watano kwa mwaka, kuuawa kwa sababu ya uhalifu, lakini Aaron anasema hii imepungua hadi wawili kwa mwaka kwa sababu vijana zaidi wanajiunga na timu yake na kuona sababu ya kujihusisha na michezo.
Anasema baadhi ya wazazi sasa wanawatuma vijana wao wachanga kujiunga na kilabu hiyo.
Vilabu vya soka vimejitokeza pia katika maeneo mengine ya makazi duni jijini Nairobi kwa nia ya kuleta mabadiliko ya kijamii miongoni mwa vijana. Timu hizi hukutana hukutana kwa michuano yao wenyewe.
Wengine hushiriki katika michezo mingine kama mpira wa wavu na chesi.
Timu ya Aaron pia imekuwa kikundi cha ustawi. Kila mwanachama huchangia nusu dola kila mwezi ambayo huenda kwa kitita na hutumika kumsaidia mwanachama kila anapopata dharura yoyote.
Anatarajia siku ambayo kijiji cha Kibarage hakitalazimika kupoteza hata mtu mmoja kwa uhalifu . George na Isichi nao wanaamini kuwa kandanda itawafungulia njia ya mafanikio maishani, na kuwapa fursa tena ya kuishi maisha mazuri.