Klabu ya soka ya Uturuki ya Galatasaray imemshtumu meneja wa Fenerbahce, Jose Mourinho, kwa kutoa "matamshi ya kibaguzi" na kuapa kuchukua hatua za kisheria dhidi yake.
Hii inafuata matokeo ya sare 0-0 katika mechi ya timu hizo mbili za Ligi Kuu ya Uturuki siku ya Jumatatu.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Mourinho alisema wachezaji wa akiba na benchi la ufunsdi la timu ya nyumbani walikuwa "wanaruka ruka kama tumbili".
Galatasaray walisema kupitia mtandao wa X kuwa Mourinho amekuwa "akitoa matamshi ya kejeli akiwalenga watu wa Uturuki" tangu alipoanza kazi ya umeneja wa timu hiyo.
"Leo, matamshi yake yamekuwa zaidi ya kukosa nidhamu na sasa yamekuwa ya kukosa utu," klabu hiyo ilisema.
"Tungependa kueleza nia yetu ya kuanzisha mchakato wa mashtaka katika vyombo vya sheria kuhusu matamshi ya kibaguzi aliyoyatoa Jose Mourinho na tutawasilisha malalamiko rasmi kwa shirikisho la soka la UEFA na FIFA."
Katika kujibu tuhuma hizo, Fenerbahce imesema matamshi ya baada ya Mourinho "yamechakachukuliwa kwa lengo la kupotosha."
"Kwa mtu yoyote mwenye akili timamu anaweza kutambua kuwa, aliyoyasema Jose Mourinho yalikuwa na lengo la kueleza namna benchi la ufundi la timu pinzani lilivyokuwa linafurahia maamuzi wakati wa mechi," Fenerbahce ilisema kwenye mtandao wa X.
Klabu hiyo imesisitiza kuwa itazingatia "haki zake za kisheria" dhidi ya "madai yasiyokuwa na msingi," ikiongeza kuwa "matamshi ya Mourinho, hayawezi kwa vyovyote vile, kunasibishwa na ubaguzi."