Na Coletta Wanjohi
Ufalme wa Buganda unasalia kuwa mojawapo ya falme chache zenye nguvu barani Afrika. Makaburi ya Kasubi ya ufalme wa Buganda yamesimama katika takriban karibu hekta 30 ya ardhi katika jiji la Kampala, nchini Uganda.
Eneo la makaburi la Kasubi lilikuwa jumba la zamani la wafalme wa Buganda. Ilijengwa na mfalme wa wakati huo Kabaka Muteesa mnamo 1882 na baadaye kugeuzwa kuwa kaburi la kifalme mnamo 1884.
Tamaduni ya Kifalme
Eneo la makaburi ya Kasubi linachukuliwa kuwa eneo la kidini na watu wa kabila la Baganda ambalo wakazi wake wanaishi eneo la kati la nchi.
Katika makaburi hayo wafalme wanne, au Kabaka kama vile wanavyoitwa katika kabila la Buganda, wamezikwa. Watoto wa kifalme pia wamezikwa huko.
Katika makaburi hayo Kabaka na wawakilishi wake pia hufanya matambiko ambayo ni muhimu kwa utamaduni wa Buganda.
Tovuti ya Urithi
"Huu ni urithi wetu, na kila kizazi kinafundisha watoto wake umuhimu wa eneo hili la kidini," anasema Sophie Nanteza, mkazi wa Kampala - mji mkuu wa Uganda.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO inaielezea kuwa kama "mahali ambapo mawasiliano na ulimwengu wa kiroho yanadumishwa."
Mnamo 2001, UNESCO lilitangaza makaburi ya Kasubi kama Tovuti ya Urithi wa Dunia.
UNESCO iliithaminiwa kama "kipengele kikuu cha ubunifu wa binadamu katika utungaji wake na utekelezaji wake, mila hai ya kitamaduni ya Baganda na kazi bora ya usanifu."
Makaburi hayo ambayo huvutia wageni wapatao 30,000 kila mwaka, yametengenezwa kwa miti ya mbao, nyasi, mwanzi na ufito katika usanifu uliobuniwa tangu karne ya 13.
"Tunaheshimu sana maeneo ya makaburi, na ni mahali pa amani," anasema Rose Mugerwa mwanamke mwenye umri wa miaka 50.
"Kila mwaka wazazi wangu huja kutoka mji wa Masaka (ambao uko zaidi ya kilomita 130 kutoka jiji la Kampala) kuja tu kuzuru makaburi, Tunaamini ni sehemu ya baraka pia" anaeleza Dan Musoke.
Makaburi yaungua
Mnamo tarehe 16 Machi 2010 fahari hii ya ufalme iliharibiwa wakati sehemu ya mahali patakatifu, iitwayo Abalongo kwenye makaburi ya Wafalme wa Buganda ilipoteketezwa na moto.
Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana, UNESCO kisha iliiweka eneo hili chini ya "Maeneo ya Urithi wa Dunia yaliyo hatarini".
"Makaburi ya kifalme ya Kasubi yaliteketezwa kwa moto mwaka 2010 lakini kazi ya kurudisha ilianza mwaka 2013. Ufalme wa Buganda na serikali ya Uganda zilifanya kazi kusimamia mchakato wa kurejesha," Charles Peter Mayiga, Waziri Mkuu wa Buganda alieleza kwa Kamati ya Urithi wa Dunia wa UNESCO katika mji mkuu wa Saudi Riyadh.
Serikali ya Uganda, Japan, Norway na UNESCO zilisaidia kurejesha hali ya makaburi haya.
Nguzo 52 zinazowakilisha koo za ufalme wa Buganda zimeshikilia paa iliyoezekwa kwa nyasi kabisa, iliyofanywa kwa utaalamu wa kitamaduni wa kiganda.
Kurudi kwa utukufu
Miaka 13 baadaye, Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO inasema maendeleo ya kurekebisha makaburi hayo yameenda vizuri na hivyo makaburi hayo yameondolewa kwenye orodha ya maeneo yaliyo hatarini kutoweka.
"Mchakato wa kurejesha ulichukua muda mrefu kwa sababu ufalme wa Buganda ulipaswa kuhakikisha kwamba desturi muhimu za kitamaduni na kiroho zinazingatiwa haraka," Mayiga alielezea, "Kazi za urejeshaji zinahitaji nyenzo muhimu za kifedha na rasilimali watu ambao kutotoridhika kunaweza kupunguza kasi," aliongeza.
Ufalme wa Buganda unasema ina nia ya kuhakikisha kuwa eneo hilo sasa linalindwa zaidi ili kuhakikisha urithi wa ufalme huo sasa hauharibiwi tena.
"Tutasimamia makaburi kwa nia ya kudumisha uhalisi wao na maadili ya kiroho ya kitamaduni," Mayiga aliiambia kamati ya UNESCO.
Kaburi hilo litafunguliwa tena kwa umma kutembelea mnamo Desemba 2023. "Tumengoja kwa muda mrefu sana kurudi kwenye eneo letu takatifu, anaelezea Musoke."
"Baba yangu alifariki ndani ya miaka 10 ya ukarabati wa makaburi lakini angalau mama yangu yu hai ili kuendelea na safari za kila mwaka za kwenda kuona eneo la makaburi," anaongezea.